Uturuki imetuma salamu za rambirambi kwa familia za wahasiriwa waliopoteza maisha wakati watu wenye silaha walipofanya shambulio dhidi ya watalii huko Kashmir inayodhibitiwa na India.
"Tunasikitika sana kujua kwamba watu wengi walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi ambalo lililenga raia katika mkoa wa Pahalgam huko Jammu na Kashmir," Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake Jumanne.
"Tunalaani shambulio hili baya."
Wizara iliendelea kusema kwamba "tunatoa pole kwa familia za waliopoteza maisha na tunawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa."
Watu wenye silaha waliwafyatulia risasi watalii katika eneo la Pahalgam, ambalo liko umbali wa kilomita 90 kwa barabara kutoka mji muhimu wa Srinagar, na kusababisha vifo vya takriban watu 26.
Waziri Mkuu Narendra Modi alishutumu "kitendo hicho kiovu" katika makazi ya majira ya joto ya Pahalgam, na kuahidi kwamba washambuliaji "watafikishwa mahakamani".
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.