Rwanda imekubali kuruhusu vikosi vya Kusini mwa Afrika vilivyokwenda kukabiliana na waasi mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwapa njia wanajeshi hao kutoka mji uliodhibitiwa na waasi wa Goma hadi Tanzania, vyanzo vitatu vya kidiplomasia vilisema Ijumaa.
Jumuiya hiyo ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yenye wanachama 16 ilisema katikati ya mwezi Machi kuwa itaanza kuondoa vikosi vyake vinavyojulikana kama SAMIDRC hatua kwa hatua kutoka Congo.
Wanadiplomasia hao watatu ambao wanafahamu yanayoendelea kuhusu mazungumzo kati ya Rwanda na SADC, walithibitisha kuwa Rwanda imekubali ombi lao kwa wanajeshi hao kupitia nchini humo kwa njia ya barabara, shirika la habari la Reuters limeriporti.
Wanadiplomasia wawili wameongeza kuwa wamefahamishwa kuwa silaha za vikosi hivyo vya kanda zitafungiwa kwa sababu za kiusalama lakini wataruhusiwa kuondoka nazo Rwanda.
Utaratibu wa kuondoa wanajeshi
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka kwa SADC wala wasemaji wa serikali za Congo au Rwanda walipoombwa kuzungumzia suala hilo.
Jenerali Rudzani Maphwanya, Mkuu wa Majeshi ya Afrika Kusini, amesema kupitia televisheni ya shirika la habari la taifa (SABC) siku ya Alhamisi kuwa timu ya wataalamu iko Tanzania kuandaa utaratibu wa kuondoka kwa wanajeshi hao.
Vikosi vya SAMIDRC vilipelekwa huko kusaidia jeshi la DRC katika kukabiliana na makundi ya waasi Disemba 2023.
Kundi la M23 limechukua udhibiti wa miji miwili mikubwa mashariki mwa Congo tangu Januari katika vita vilodumu kwa muda mrefu ambavyo chimbuko lake ni mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 na pia kugombania raslimali za Congo.