Kulingana na historia na tamaduni ya Kanisa Katoliki, inapotokea kifo cha kiongozi wa kanisa hilo duniani, ambaye ni Papa, basi mwili wake huzikwa ndani ya majeneza matatu.
Kwanza, mwili wake uhifadhiwa kwenye jeneza la miberoshi au cypress. Hii inaashiria unyenyekevu.
Baadae, mwili wake uhamishwa kwenye jeneza la chuma, ili kuukinga mwili huo.
Hatimaye, jeneza la pili linawekwa ndani ya jeneza la nje la mwisho lililotengenezwa na mwaloni au oak, kuashiria utu na nguvu.
Hata hivyo, Papa Francis ambaye atazikwa Aprili 26, 2025 alikiuka taratibu hizi za maziko, kupitia mabadiliko aliyoyafanya mwaka 2024.
Kupitia wosia wake, Papa Francis alitaka mwili wake uwekwe kwenye sanduku moja la kawaida, lililotengezwa kwa mbao kwa upande wa juu, na ndani yake liwe na madini ya zinki.
Mwili wa Papa utavalishwa mavazi mekundu ya kilitrujia, kofia kubwa maarufu kama mitre na kanzu yake ya Kiaskofu.
Kitambaa cheupe kitawekwa juu ya uso wa Papa na usiku kabla ya mazishi, jeneza litafungwa mbele ya makadinali wengine wakuu.
Mfuko wenye sarafu zilizotengenezwa wakati wa upapa wake utawekwa ndani ya jeneza pamoja na ukurasa mmoja ulioandikwa wa upapa wake - unaojulikana kwa Kiitaliano kama "rogito," neno linaloonyesha hati rasmi.
Alipendekeza kuwa kaburi lake lisipambwe ila liwe tu na maandishi yanayosema:" Franciscus."