Taifa hilo limekuwa na kiongozi mmoja wa nchi tangu mwaka 1986. Rais wa Uganda ni Yoweri Kaguta Museveni.
Rais Museveni alizaliwa miaka 80 iliyopita eneo la Ntungamo nchini Uganda. Alipata mafunzo yake ya elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania ambapo alijikita katika sayansi ya siasa.
Mwaka 1972 alishiriki katika jaribio la mapinduzi dhidi ya rais Idi Amin, ambalo halikufanikiwa.
Mwaka uliofuata akaunda kundi la wapiganaji Front for National Salvation (FRONASA) na kushirikiana na wanajeshi wa Tanzania katika vita vya Tanzania na Uganda vilivyomalizika kwa kumpindua Amin.
Mwaka 1980 akagombea urais akiwa na chama cha Uganda Patriotic Movement, lakini akadai kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki baada ya kushindwa na Milton Obote.
Alijipanga upya akiunganisha upinzani chini ya National Resistance Movement na kuanzisha vita vya msituni.
Kufikia Januari 1986 na baada ya vita vya Kampala, Museveni aliapishwa kuwa rais wa taifa hilo. Kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kuuzima uasi ambao ulitishia utawala wake na mfumo wa Uganda.
Pamoja na hayo haikuwa rahisi kueneza uongozi wake kote nchini Uganda, kukiwa bado na makundi ya wapiganaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Baada ya muda akafanikiwa kudhibiti nchi nzima huku baadhi ya viongozi wa wapiganaji wakiamua kujiunga na serikali yake na kupewa wadhifa.
Baada ya Museveni kushika uongozi uchaguzi wa kwanza Uganda ulifanyika 1996 ambapo alishinda. Akapata tena ushindi 2001 dhidi ya mshirika wake wa zamani Kizza Besigye.
Katiba ikabadilishwa kuondoa ukomo wa mihula 2005 na ukomo wa umri 2017. Aliwahi kusema kuwa 2001 ingekuwa mwisho wake kugombea urais, lakini kwa mabadiliko hayo ikamaanisha ataendelea kushiriki.
2006 ikawa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi nchini Uganda. Yoweri Museveni alishinda uchaguzi huo, akagombea tena 2011, 2016, 2021 mara zote akipata ushindi na upinzani wakilalamika uchaguzi kutokuwa huru na haki.
Sasa hivi tayari amethibitisha kuwa atagombea tena uchaguzi wa mapema mwaka 2026. Itakapofika wakati huo atakuwa ametimiza miaka 40 kamili uongozini na akiangazia kuongeza kipindi hicho.
Rais Museveni mwenyewe anasema ni kutokana na umaarufu alionao na kupendwa na watu ndiyo maana amechaguliwa miaka nenda, miaka rudi.