Mechi ya fainali ya ligi ya mataifa ya Ulaya ya mwaka huu ilikuwa kati ya Ureno na Hispania na Ureno ikafanikiwa kulibeba taji hilo kwa mara ya pili baada ya kuwafunga Hispania kupitia mikwaju ya penati. Timu hizo zilikuwa zimetoka sare ya 2-2 katika muda wa kawaida.
Mchezaji bora wa mechi hiyo alikuwa ni kijana wa Ureno Nuno Mendes ambaye pia alimpa tabu sana mchezaji wa Hispania kinda mwingine Lamine Yamal.
Nuno Alexander Tavares Mendes ni beki wa timu ya taifa ya Ureno na pia anacheza katika klabu ya mabingwa wa bara Ulaya PSG ya Ufaransa.
Amezaliwa miaka 22 iliyopita eneo la Sintra, jijini Lisbon, Ureno na ana asili ya Angola.
Alianza kucheza soka akiwa katika timu ya vijana ya Sporting na mara ya kwanza kucheza kwa timu ya wakubwa ilikuwa mwaka 2020 na msimu uliofuata wakashinda ligi kuu ya Ureno Primeira Liga na kombe la Taca da Liga.
Nuno Mendes akawa bado wa moto na mwaka 2021 akajiunga na PSG kwa mkopo, ila mwaka 2022 akamakinika huko kabisa.
Katika kucheza kwake alianza kama kiungo mshambuliaji na baadaye beki akiwa na klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno.
Akiwa na timu ya taifa pia alicheza kwa upande wa vijana kabla ya kujitosa kwenye kikosi cha kwanza cha taifa akianza katika timu hiyo mwaka 2021.
Pia alichaguliwa kwa kikosi cha kombe la dunia mwaka 2022 na mara mbili akawa kwenye kikosi cha mashindano ya bara Ulaya.
Katika mechi yao ya 8 Juni Ureno dhidi ya Hispania baadhi ya wachambuzi wanasema ndiyo alikuwa tiba na mwiba wa kinda wa ‘La Roja’ Lamine Yamal, kwa kifupi alimuweka mfukoni kijana machachari Lamine Yamal.
Kuchaguliwa kwake kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, haikuwa kwa kubahatisha. Alifanikiwa kuisawazishia Ureno goli.
Ameipa hadhi nafasi ya mabeki na anacheza timu moja na mkongwe, mkali wa hizi kazi Cristiano Ronaldo.
Je, tutarajie makubwa zaidi kutoka kwa kinda Nuno Mendes?