Unapozunguuka katika vichochoro vya Mji Mkongwe kisiwani Unguja, utaona idadi kubwa ya mabinti wamekaa vibarazani na vifaa vyao vya uchoraji hina. Hapo wanakuwa wanategea wateja wanaopita katika vichochoro hivyo, na mara nyingi huwa ni watalii wanaotoka maeneo mbalimbali ikiwemo ndani na nje ya nchi.
Mmoja wa mabinti hao ni Zuwena Abdallah, binti wa kizanzibar aliyejiajiri kupitia fani hiyo ya uchoraji hina.
Katika mazungumzo yake maalumu na TRT Afrika, ameelezea jinsi alivyoanza kujiingiza katika uchoraji wakati bado ni mwanafunzi wa sekondari. Baada ya mtihani na kushindwa kuendelea na masomo ya ngazi ya juu, hapo ndipo alipoamua sasa kujikita zaidi katika uchoraji.
"Na hapo ndipo nikaamua kuingia kwenye uchoraji hina kama kazi ambayo inaniwezesha kupata pesa ili niende kusoma chuo," anasema Zuwena.
Pia aliweka wazi kwamba, biashara yao inategemea zaidi kuwepo kwa wimbi kubwa la wageni wanaoingia visiwani humu.
Zuwena anasema kipato chake cha wastani kwa mwezi ni sawa na dola 120.
‘‘Nilipomaliza kusoma ndio nikaingia huku kwenye hina kwa sababu nilikuwa sina pesa ya kwenda chuo,’’ alisema Zuwena.
Mbali na Zuwena, kuna wanawake wengi tu sehemu tofauti katika mwambao wa pwani ya bahari ya Hindi ambao wameajiajiri kama wachoraji wa hina na wapambaji wa maharusi na shughuli mbali mbali katika tasnia ya urembo.
Kwa nini vijana wengi wa kike wanajifunza kuchora hina?
Kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wa eneo la Afrika Mashariki, kama ilivyo katika maeneo mengine, nchini Tanzania kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wanaojifunza fani ya uchoraji hina kwa lengo la kujipatia kipato.
Mafunzo haya mara nyingi hutolewa na watu binafsi lakini pia kuna taasisi ambazo zimeanzishwa kukuza vipaji vya uchoraji hina.
Akiongea na TRT Afrika, Hassan Kimbwembwe, ambae ni Mtendaji Mkuu wa kituo kinachoitwa Helping Hand for Relief and Development Tanzania-HHRD amesema hii inasaidia vijana kujipatia ajira wao wenyewe baada ya kupatiwa ujuzi. Kwa mujibu wa Kimbwembwe, mbali na vijana hawa kupata mafunzo, lakini pia, wanapomaliza masomo na kufaulu vizuri, basi kuna fursa ya kupata mitaji ya kuanzisha biashara zao‘
‘‘Lengo kubwa hasa ni kuwapa vijana ujuzi ambao, watakuwa wanaenda kuzalisha baada ya kutoka hapa,’’ anasema Kimbwembwe.
Naye Biban Dewji, ambae ni mwalimu wa hina katika kituo cha kukuza ujuzi wa vijana cha HHRD jijini Dar es Salaam amesema, "Kijana yeyote anapojua fani tofauti tofauti anaweza kuwasaidia vijana wengine na wao wakaweza kujiajiri. Kwa sababu mimi ni mwalimu lakini pia nafundisha wanafunzi na wao pia wakija kujua vizuri watakuja kufundisha wanafunzi wenzao.’’
Waalimu na wataalamu wa kuchora hina wanasema mtu anayetaka kujifundisha sanaa ya hina basi yeye ndie huwa muamuzi. Akiwa ni mwenye bidii na hima basi ndani ya mwezi au miezi miwili anaweza kuwa tayari na kuanza kuchora watu. Lakini akiwa mzito wa kufahamu basi anaweza kuchukua muda mrefu kiasi cha hata mwaka mmoja na bado akawa anaendelea kujifunza tu.
Hina ina madhara gani kwa afya ya binadamu
Kwa mujibu wa waalimu, wataalamu wa afya pamoja na watumiaji wa hina hakuna madhara ya kiafya ambayo yamethibitka kutokana na matumizi hina.Hali ambayo ni kinyume na watumiaji wa michoro ya piko. Kwani watu wengi wamekuwa wakipata madhara kwenye ngozi baada ya kuchora kwa kutumia piko ambayo hutengenezwa ka mchanganyiko wa kemikali.Mchanganyiko wa unga wa hina, limau na maji pekee huifanya hina kuwa ni ya kiasili zaidi hata kuwa dawa ya kusaidia kukuza nywele.Michoro ya hina inafanana na ile ya tatoo lakini hufutika baada ya muda jambo ambalo ni gumu kwa upande wa tatoo.
‘‘Nilianza kuchora kidogo kidogo nilipokuwa bado nasoma. Nilipomaliza kusoma ndio nikaingia huku kwenye hina kwa sababu nilikuwa sina pesa ya kwenda chuo."
Fani ya uchoraji hinna inaendelea kukua kila siku. Ingawa asili yake ni mwambao wa Afrika Mashariki, lakini tamaduni hii hivi sasa inaonekana kuenea katika maeneo mengine mbali na ukanda huo.
Kwa karne kadhaa, uchoraji wa hina umekuwa ni sehemu muhimu katika mapambo ya mwanamke. Panapokuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo harusi, au hata katika sherehe za sikukuu, utaona wanawake wa rika mbalimbali wakijishughulisha kuchorwa kuanzia mikononi mpaka miguuni. Mara nyingi uchoraji wake unakuwa ni wa nakshi ambayo ni maua ya aina mbalimbali yanayovutia.
Urembo wa kuchora hina umepiga kasi hasa kwenye miaka ya hivi karibuni. Na hii ni baada ya kubuniwa kwa aina mbali mbali za mitindo ya uchoraji wa nakshi na maua yanayoakisi ubunifu wa mchoraji.