AFRIKA
4 DK KUSOMA
Wanawake Burundi wachangamkia fursa za ajira zinazofanywa na wanaume
Katika hali isio ya kawaida wanawake wameanza kuchangamkia kazi ambazo awali ziliaminika kuwa ni za wanaume.
Wanawake Burundi wachangamkia fursa za ajira zinazofanywa na wanaume
  Chimaine Nshimirimana  kutoka Burundi aelezea jinsi alivyokiuka mtizamo wa jamii na kufanya kazi zilizozoeleka kufanywa na wanaume. / Others
27 Oktoba 2023

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Katika hali isio ya kawaida wanawake wameanza kuchangamkia kazi ambazo awali ziliaminika kuwa ni za wanaume. Huko Burundi baadhi ya kampuni za usafiri wa basi zimeanza kutoa ajira kwa wanawake kadhaa kama madereva au ''makonda'' wa bus, ambao shughuli yao kubwa ni kuwaita na kuwakaribisha abiria pamoja na kuwalipisha nauli. Miongoni mwa wanawake waliopata fursa hiyo, ni pamoja na Chimaine Nshimirimana ambae amejipatia umaarufu wa ghafla na kuvutia wengine wanaomuona kama mfano.

Chimaine Nshimirimana baada ya kumaliza shule yake ya upili katika fani ya ''Computer Sciences'' alijikuta bila ajira kwa zaidi ya miaka minne na hivyo ikamlazimu kuchangamkia fursa iliopatikana ya kufanya kazi ya ukonda katika moja wapo ya kampuni za usafirishaji mjini Bujumbura.

Hata hivyo, anakiri kwamba, mwanzo haukuwa rahisi kutokana na uoga aliokuwa nao. Nilikuwa sijazoea kusimama wakati gari inatembea tena ikiwa ina abiria. Isitoshe, nilikuwa na aibu sana ya kuwaita watu abiria kwa 'kupiga debe' na hata kuwalipisha nauli.''

''Nakumbuka nilimlipisha mtu nikarudi, baadae kidogo nikarudi tena kumlipisha. Akaniambia dada nilishakulipa. Kumbukumbu nyingine, kuna siku nilianguka. Dreva wangu alijua tayari nimeshapanda gari kumbe nilikuwa nje. Hivyo nikaburuzwa kidogo nikaumia sana miguuni,'' anasimulia Chimaine.

Lakini yote sasa hayo yamepita na Chimaine amekuwa mzoefu katika kazi yake, ''Nashkuru Mungu sasa nimeanza kuzoea. Naweza kujua na kutunza kumbukumbu ya waliolipa na ambao bado, na wale waliopanda njiani pia."

Lakini mtihani kwa Chimaine haukuwa tu kuzowea kazi, lakini pia namna jamii itavyomchukuliwa. Kwanza kabisa aina ya kazi anayofanya imezoeleka nchini Burundi kufanywa na wanaume, hii ni kutokana na mila na tamaduni za Warundi ambayo inawazuia wanawake kufanya kazi za aina hiyo. Lakini kutokana na ujasiri wake, aliukiuka mtazamo huo wa jamii.

''Mara ya kwanza nilipowaambia watu kuwa nimepata kazi kwenye Kampuni ya usafirishaji hawakunielewa. Waliniambia sitaweza kwa sababu ni kazi ya wanaume. Walikuwa na hofu ya ajali na kwamba ni kazi yenye mikiki mikiki kutokana na foleni za watu kwenye vituo. Nikawaambia naenda kujaribu. Sasa hivi, nashukuru Mungu jamii imeanza kutuelewa 'makonda wanawake.'' Ukikutana na watu utasikia wakinipongeza na kuniambia nipambane. Kuwa na bidii. Na hii inatutia moyo sisi wanawake tunaofanya kazi hii.''

''Mara ya kwanza nilipowaambia watu kama nimepata kazi kwenye Kampuni ya usafiri hawakunielewa. Waliniambia hautaweza ile ni kazi ya wanaume. Walikuwa na hofu ya ajali au kwamba ni kazi ya mikiki kutokana na foleni za watu kwenye vituo. Nikawaambia mie nakwenda kujaaribu najua tu nitaweza. Sasa hivi nashkuru Mungu wana jamii wameanza kutuelewa 'makonda wakike.'

- Chimaine Nshimirimana, konda mwanamke Burundi

Hata hivyo, kama ilivyo kwenye kazi nyengine, changamoto siku zote hazikosekani.

''Unaweza kuwa na abiria mlevi. Wakati wa kulipia inakuwa shida. Wakati mwengine anakupa pesa pungufu. Wengine wanajaribu kuonyesha' mabavu' wakidai sisi ni wanawake tu. Lakini ndio mitihani ya kazi,'' anasema Chimaine.

Chimaine Nshimirimana licha ya kazi ya 'ukonda' ni mama wa familia yenye watoto watatu. Hivyo, kazi yake licha ya kumsaidia kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya familia, lakini pia muda mwingi anakuwa mbali na watoto wake.

"Mara nyingi naenda kazini alfajiri, watoto wanakuwa bado hawajaamka. Narudi saa tatu usiku watoto wakiwa wamelala. Nakosa muda wa kuwaona watoto. Na hili kwa kweli linanitesa kabisa. Hakuna muda wa kuongea n'a watoto. Lakini ndio hivyo, nawatafutia hao hao ili kustaawisha maisha yao,'' anasema.

Chimaine anawatia moyo wanawake wengine wanaopitia changamoto kama hizo kuwa na ujasiri wa kufanya kazi hata ambazo zimezoeleka kufanywa na wanaume.

"Maisha ni kusaidiana. Haiwezekani kumuachia mwanamume kila kitu. Maisha yamebadilika," anasema.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us