Na Pauline Odhiambo
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Tasisi iliyoanzishwa na binti mdogo aliyezaliwa na ‘mdomo sungura’ yapania kuondoa unyanyapaa kwa watu wenye hali hiyo huku ikiazimia kuonesha umuhimu wa kuchangia matibabu yake.
Sehemu ya alama iliyosalia kwenye sehemu ya juu ya kinywa chake, sio aibu kwa Seitebogo Peta.
Kimsingi, anajisikia fahari sana kubaki na alama hiyo mwilini wake.
Ingawa upasuaji wa mwisho kwenye kinywa chake ungeweza kuondoa kumbukumbu za mateso aliyopitia utotoni, Seitebogo anaona bora kuwa na tabasumu lake lenye kubeba kasoro, kile anachoelezea kuwa ni ‘sehemu muhimu ya maisha yake.’ Akiwa amezaliwa na ‘mdomo sungura,’ hali ya kuwa na uwazi ama nafasi katika mdomo wa juu jirani na pua, Seitebogo amekwishafanyiwa upasuaji kadhaa kurejesha tabasamu usoni mwake.
Ilimlazimu binti huyo mwenye umri wa miaka 32 kupambana na namna jamii na dunia kwa ujumla invyowachukulia watu wenye midomo sungura.
Hilo bado halikumrudisha nyuma Seitebogo katika harakati za kuwapambania wenzake. Kupitia Taasisi ya Seitebogo Peta, aliyoianzisha mwaka 2017, binti huyo amejitahidi kurejesha tabasamu nyingi kwa watu wenye hali kama aliyokuwa nayo.
“Niliangazia makundi yote mara tu baada ya kuanzisha taasisi hii,” anasema Seitebogo katika mahojiano maalumu na TRT Afrika. “Nilionekana kuguswa zaidi na watoto, mara baada ya kushika mimba.”
Seitebogo anakiri wazi kuwa huenda binti yake angerithi hali hiyo kutokana na sababu za kijenetiki, sababu kuu inayotajwa pia na Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Baada ya binti yangu kuzaliwa mwaka 2019, kitu cha kwanza kuangalia ilikuwa ni kinywa chake,” anaelezea. "Nilifarijika sana kuona kuwa hakuwa na hali hiyo ingawa nilijaribu kuvaa viatu vya wazazi wenye watoto wenye midomo sungura.”
Uhusiano wa kimafamilia
Kwa mujibu wa WHO, hakuna mahusiano ya moja kwa moja ya jenetiki yanayosababisha hali hii. Hata hivyo, WHO inadai kuwa kuna wakati yapo na wakati mwengine hakuna.
Kati ya sababu za kimazingira, kwa mujibu wa Shirika hilo, ni kwa kina mama wajawazito kutumia dawa maalumu, kabla ya kujifungua, uvutaji wa sigara, unywaji pombe na mkao wa mtoto ndani ya tumbo la uzazi.
Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, kuna uwezekano kwa watoto walipangiliwa, na kuzaliwa wakiwa na siha njema kupata ‘midomo ya sungura’.
“Baadhi ya watu hapa Afrika ya Kusini, wanahusisha hali hiyo na ushirikina au adhabu ya Mungu kutokana na makosa ya wazazi,” anaelezea Seitebogo.
“Baadhi ya watu hapa Afrika ya Kusini, wanahusisha hali hiyo na ushirikina au adhabu ya Mungu kutokana na makosa ya wazazi,” anaelezea Seitebogo.
Makovu yenye hisia
Kulingana na wataalamu wa afya, mtoto mchanga anaweza kuzaliwa na mpasuko kwenye mdomo wa juu na kuathiri upande mmoja wa uso ama pande zote.
Lakini kwa hali kama iliyomtokea Seitebogo, yote yanawezekana.
Kufuatia hali hiyo, ilimlazimu binti huyo kufanyiwa upasuaji kadhaa kurekebisha sura yake ya utotoni.
Dhihaka Shuleni
Kwa hakika, ilimuwia vigumu Seitibogo kuishi na ‘mdomo sungura,’ hasa akiwa shuleni kutokana na dhihaka alizopata kutoka kwa wanafunzi wenzake.
"Nilikuwa ni mwanafunzi mwenye kujiamini sana, nakumbuka nikiwa shule ya msingi, nilipishana hoja na mwanafunzi mmoja aliyejaribu kunifananisha na mbwa kwenye moja ya vipindi vya televisheni,” anaeleza.
Dhihaka na utani wa mara kwa mara shuleni ulimuondolea hofu Seitebogo, na kimsingi kumfanya kudiriki kuitetea hali yake, kwa namna yoyote ile.
"Baada ya binti yangu kuzaliwa, nilianza kuhofia namna atakavyoishi na kupambana na utani na dhihaka,” anaeleza.
Mzigo mkubwa
Pamoja na unyanyapaa aliokumbana nao, Seitebogo safari za mara kwa mara hospitali, zilikuwa ni sehemu ya maisha ya binti huyo.
“Inamlazimu binadamu yoyote aliyezaliwa na mdomo sungura kuwa karibu na wataalamu wa afya kwa wakati wote,” anasema. "Mara uko na mtaalamu huyu mara yule, hakika ni pilipapilika yenye kuchosha."
Hata hivyo, bado Seitebogo anajiona mwenye bahati sana kwani wazazi wake waliweza kugharamia matibabu yake.
"Ni ngumu sana kwa raia wengi wa hapa Afrika ya Kusini kugharimia matibabu hayo," anasema. Changamoto hiyo ilimsukuma Seitebogo kuongeza wigo wa shughuli za taasisi ikiwemo kusaidia familia zenye kipato cha chini kupata huduma za afya wanazohitaji zaidi.
"Mara nyingi, najihusisha na wazazi waliokata tamaa na matibabu ya midomo sungura kwa watoto wao," Seitebogo anasema. “Baadhi, wamediriki hata kuwatelekeza watoto waishio na hali hiyo kutokana changamoto za kifedha.”
Tabasamu linalovutia
Hadi sasa, Seitebogo, kupitia taasisi yake ameweza kuwafikia zaidi ya watu 50 kupata huduma za urekebishwaji, wengi wakiwa ni watoto. "Baadhi wamekuwa wakitokea sehemu za mbali, kama vile Eastern Cape, Kwazulu Natal na Northwest. Pia niliweza kumsaidia mwanamke mwenye miaka 25, na nilifarijika kuona akirejea kwenye hali yake ya kawaida,” anasema.
"Kitu muhimu kwangu, ni kurejesha tabasamu kwa wagonjwa waliokwisha kata tamaa.”
Ni matumaini ya kupanua wigo wa shughuli za taasisi yake, kujumuisha pia urekebishwaji wa sura kwa makundi yote, na kutoa huduma za afya zifaazo, wakati wote.