AFRIKA
3 DK KUSOMA
Ugonjwa wa macho mekundu wahamia pwani ya  Kenya
Dalili za 'Red Eyes' zimeripotiwa katika shule nyingi kwenye ukanda wa pwani ya Kenya, huku mamlaka zikizitaka taasisi hizo kukabiliana vilivyo na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa macho mekundu wahamia pwani ya  Kenya
Mmoja ya waathirika wa ugonjwa wa 'Red Eyes' ulioikumba pwani ya Kenya./Picha: TRTAfrika / Others
24 Januari 2024

Fathiya Bayusuf

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Idara ya huduma za afya katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya, imezitaka taasisi za elimu eneo hilo kuzingatia kanuni za usafi baada ya kuripotiwa kuzuka kwa ugonjwa wa macho mekundu.

Mamlaka hiyo imetoa rai kwa uongozi wa taasisi hizo kuzingatia kanuni bora za afya kama vile kunawa kwa kutumia maji titirika na sabuni, kutumia vitakasa mikono na kwenda hospitalini pindi wanapohisi dalili za ugonjwa huo.

"Idara ya hudumu za afya ingependa kuufahamisha umma juu ya dalili za uwepo wa ugonjwa wa macho mekundu unaosambaa kwa kasi," ilisema sehemu ya taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo.

Kulingana na mamlaka hiyo, dalili za ugonjwa huo ambao pia uliikumba pwani ya Tanzania, hasa maeneo ya Dar es Salaam, katika siku za hivi karibuni, zinajumuisha kuumwa, kuwashwa na kuvimba kwa macho.

"Mwanafunzi atayekuwa na dalili za namna hii, hatoruhusiwa kuendelea na masomo mpaka itakapothibitika kama amepata tiba ya haraka," taarifa hiyo iliongeza.

Kwa upande mwingine, tahadhari hii imeleta taharuki kwa wanafunzi wengi wa eneo hilo, wengi wao wakifurika katika vituo vya afya kutafuta tiba yake.

Hajj AbdulHakim, mmoja wa wanafunzi kutoka eneo hilo anadai kupatwa na dalili za ugonjwa huo na uongozi wa shule ukampa ruhusu ya kwenda kituo cha afya kwa ajili ya kupata matibabu.

"Nilianza kuwashwa jicho langu asubuhi na baada ya masaa machache likawa jekundu zaidi. Nilipoanza kuhisi kama jicho linataka kutoka, ndipo nikagundua nina shida. Nililazimika kukaa nyumbani na kutafuta matibabu. Nashukuru naendelea kupata nafuu," anasema.

Hajj anakiri kutengwa na wenzake baada ya kupata dalili za maradhi hayo, jambo lililomlazimu yeye mwenyewe kujitenga na kuamua kwenda hospitali.

Walimu nao hawakusalimika na ugonjwa huo.

Elye Abbas anaeleza namna alivyoendelea na kazi zake, akijitahidi kutochangamana na walimu wenzake.

"Nilianza kuwashwa na macho yangu na nikabaini niliambukizwa ugonjwa huo na wanangu waliokuja nao kutoka shuleni. Tulitafuta matibabu, na sasa tunaendelea vizuri."

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us