DRC, mzalishaji mkubwa zaidi wa kobalti duniani
DRC, mzalishaji mkubwa zaidi wa kobalti duniani
DRC ndio kinara wa uzalishaji wa madini haya duniani. Takwimu zinaonyesha kwamba, nchi hiyo inachangia zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji wa kobalti duniani.
27 Juni 2025

Afrika ina utajiri mkubwa wa madini ya kobalti na kuiweka katika sehemu ya juu duniani kwa uzalishaji wa madini haya. Kobalti ni muhimu katika utengenezaji betri za
lithiamu muhimu kwa magari ya umeme na vifaa vya kielektroniki.

Madini haya yamepata mahitaji makubwa yanayotokana na kuongezeka kwa teknolojia ya nishati safi, wakati mabadiliko ya ulimwengu yakielekea kwenye suluhisho ya nishati endelevu.

Barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ( DRC ), Morocco, Zambia, Afrika Kusini na Madagascar ni miongoni mwa nchi zinazozalisha kobalti.

Hata hivyo, DRC ndio kinara wa uzalishaji wa madini haya duniani.

Takwimu zinaonyesha kwamba, nchi hiyo inachangia zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji wa kobalti duniani kwa mwaka 2024.

Mwaka huo uzalishaji wa kimataifa wa kobalti ulifikia tani 290,000, huku takriban tani 220,000 zikitoka DRC.

Hii ilichangiwa na migodi ya Kisanfu na Tenke Fungurume. Hata hivyo, uchimbaji madini unafanywa na wajisiriamali wadogo wadogo bila kutumia teknolojia ya kisasa. Lakini kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa kawaida ambao wanadai kutonufaika na sifa ya nchi yao kuwa kinara wa uzalishaji wa madini hayo.

Sekta hiyo ya madini ya kobalti mpaka sasa inaripotiwa kuajiri takriban watu milioni 12.5.

Huku ripoti kadhaa zikiangazia wasiwasi wake juu ya athari za kijamii na kimazingira za uchimbaji wa kobalti, hii ikijumuisha tuhuma za wimbi la watoto wanaodaiwa kutumikishwa katika migodi bila kuzingatia usalama wao.

Bei ya kobalti inapungua

Lakini sasa DRC imechukua hatua ya kuboresha sekta na mapato kwa wananchi wake. Februari 2025, ilisimamisha kwa miezi minne mauzo ya nje ya kobalti.

Mwezi Juni imeongeza marufuku hiyo tena kwa miezi mitatu.

“Uamuzi umechukuliwa kuongeza muda wa kusimamishwa kwa muda kutokana na kuendelea kwa kiwango kikubwa cha hisa kwenye soko," Mamlaka ya Udhibiti wa Masoko ya Kimkakati ya Bidhaa za Madini (ARECOMS) ilisema katika taarifa yake.

Imesema lengo ni kuzuia usambazaji holela wa madini hayo.

Hii ni baada ya bei ya kobalti kugonga $10 tu kwa pauni ikishuka kutoka kwa dola 23 kwa pauni mwaka 2024.

Serikali hiyo imesema inataka muda zaidi wa kutafuta njia ya kusambaza mgao wa mauzo ya nje miongoni mwa makampuni ya madini.

Inachukua takriban siku 90 kusafirisha bidhaa ya kati ya Kobalti ya DRC hadi Uchina ili kusafishwa, kumaanisha athari kamili ya marufuku ya usafirishaji ya Februari imecheleweshwa.

Takwimu zinaonyesha uagizaji wa China wa kobalti ya DRC ulibakia kuwa thabiti kwa zaidi ya tani za metric 50,000 mwezi Machi na Aprili.

Zaidi ya hayo, bado China ina kiwango kikubwa cha kobalti kutokana na madini mengi ya kobalti kwenye soko wa miaka iliyopita.

Kobalti ya DRC ni zao la shaba, chuma muhimu kinachohitajika katika matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na njia za kusambaza na kuzalisha umeme.

Wakati mauzo ya nje ya shaba yanaendelea bila kukoma, wazalishaji wa kobalti hawana budi ila kuhifadhi madini hayo kwenye maghala.

Hata hivyo, watalaam wanasema uamuzi huo ulifanikiwa kusukuma bei ya kobalti duniani lakini ulisababisha mrundikano wa madini hayo ndani ya DRC na kubana hazina ya serikali.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us