AFRIKA
3 DK KUSOMA
Mmoja auwawa, zaidi ya 200 wajeruhiwa katika maandamano ya kupinga muswada wa fedha nchini Kenya
Mtu mmoja amepoteza maisha na zaidi ya 200 kujeruhiwa nchini Kenya kufuatia maandamano ya kupinga ongezeko la kodi nchini Kenya, siku ya Alhamisi.
Mmoja auwawa, zaidi ya 200 wajeruhiwa katika maandamano ya kupinga muswada wa fedha nchini Kenya
Polisi nchini Kenya wakipambana na waandamanaji wakati wa vurugu za kupinga muswada wa fedha katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi /Picha: AFP / Others
21 Juni 2024

Mtu mmoja ameuwawa na wengine 200 kujeruhiwa siku ya Alhamisi, kufuatia maandamano ya nchini nzima yenye kupinga hatua ya serikali ya nchi hiyo kuongeza mzigo wa kodi hadi kufikia dola bilioni 2.7, wanaharakati wa haki za binadamu wamesema.

Polisi walifyatua mabomu ya machozi kuwatanya waandamanaji hao katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi, kulingana na taarifa iliyotolewa na Chama cha Madaktari nchini Kenya na Amensty International.

Katika taarifa yao, taasisi hizo mbili zilidai kuwa maganda ya risasi zilizotumika zilidhihirisha matumizi ya silaha wakati wa maandamano hayo, na kuongeza kuwa zaidi ya waandamanaji 100 wamekamatwa nchi nzima.

Siku ya Ijumaa, chombo huru cha kuchunguza mienendo ya Polisi nchini Kenya (IPOA), kilisema kuwa kimeorodhesha kifo cha mtu mmoja "anayedaiwa kuuwawa na polisi na majeruhi wengine wengi wakiwemo polisi wenyewe wakati wa maandamano hayo."

Wito wa kuukataa muswada wa fedha

Mtu huyo, anayekadiriwa kuwa na miaka 29 alipoteza maisha wakati anapokea matibabu ya jeraha kwenye mguu wake siku ya Alhamisi usiku, kulingana na ripoti ya polisi. Hata hivyo, ripoti hiyo haikuweka bayana namna alivyoshambuliwa na kujeruhiwa.

Kwa upande wake, kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi Adamson Bungei hakuwa tayari kupokea simu.

"Tunawapongeza maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa ni vijana kwa kuamua kuandamana kwa amani licha ya kusumbuliwa na polisi," walisema wanaharakati hao.

Waandamanaji hao wanaitaka serikali kutopitisha muswada huo wa fedha, wakidai kuwa utaathiri uchumi na kuongeza gharama za maisha kwa wakenya wengi.

Rais alegeza msimamo

Shirika la Fedha Duniani linasema kuwa serikali ya Kenya inahitaji kuongeza vyanzo vya mapato ili kupunguza ombwe la bajeti na hali ya kukopa.

Mwanzoni mwa wiki, serikali ililegeza kidogo msimamo wake, huku Rais William Ruto akiidhinisha mapendekezo ya kuondoa baadhi ya kodi mpya ikiwemo ya umiliki wa gari, mikate, mafuta kupikia na miamala ya fedha.

Licha ya maandamano hayo yaliyofanyika katika kaunti 19 kati ya 47 nchini Kenya, watunga sheria walipitisha muswada huo baada ya kusomwa kwa mara ya pili siku ya Alhamisi, ukisubiri kuwa sheria.

Wabunge hao wanatarajiwa kukutana siku ya Jumanne kupigia kura baadhi ya mapendekezo ya kwenye muswada huo.

Pata habari zaidi kupitia whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us