ULIMWENGU
2 DK KUSOMA
Rais Samia aagiza uchunguzi wa kina mauaji ya mjumbe wa CHADEMA
Kiongozi huyo wa Tanzania pia ameviagiza vyombo vya uchunguzi nchini humo kumpelekea taarifa kuhusu tukio hilo.
Rais Samia aagiza uchunguzi wa kina mauaji ya mjumbe wa CHADEMA
Rais / Others
8 Septemba 2024

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya uchunguzi vya nchi hiyo kufuatilia kwa kina kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Sekretariati ya chama cha CHADEMA, Ally Mohamed Kibao.

Akionesha kusikitishwa na kifo hicho, Rais Samia pia ameagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo na mengine ya namna hiyo kwa haraka.

"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya mauaji ya kiongozi wa CHADEMA Bwana Mohamed Ali Kibao. Natoa pole kwa viongozi wa chama hicho, familia ya Mzee Kibao, ndugu, jamaa na marafiki," alisema Rais Samia katika chapisho lake kwenye ukurasa wa X.

Kulingana na Rais Samia, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kila raia ana Haki ya kuishi, huku akisisitiza kuwa serikali anayoingoza haitovumilia vitendo vya kikatili kama hivyo.

Mwili wa Kibao ulipatikana katika eneo la Ununio jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali na kwenda kuhifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Mwananyamala, kabla haujatambuliwa na ndugu zake, wakiwemo pia viongozi wa CHADEMA, waliokuwa wanaongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe, siku ya Septemba 8, 2024.

Mwanachama huyo wa CHADEMA aliripotiwa 'kutekwa' na watu wasiojulikana akiwa ndani ya basi siku ya Septemba 6.

Siku moja baadaye, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limesema kuwa limeanza uchunguzi wa taarifa za ‘kutekwa’ kwa Kibao ambaye ni Mjumbe wa Sekretarieti wa CHADEMA, kabla ya mwili wake kupatikana katika hospitali ya rufaa ya Mwananyamala.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us