AFRIKA
2 dk kusoma
Kenya kuondowa paa za asbestosi
Asbestosi, ilitumika sana katika ujenzi nchini Kenya katika miaka ya sitini na sabini, na bado imebaki katika majengo ya serikali, hospitali, shule, na hata katika ujenzi wa mifumo ya maji.
Kenya kuondowa paa za asbestosi
Shirika la Afya Duniani linasema asbestosi ina madhara ya kiafya kama saratani/ picha: Getty / Getty Images
11 Machi 2025

Baraza la Mawaziri la Kenya limeidhinisha mpango wa kuondolewa kwa paa aina ya asbestosi kutoka kwa majengo ya umma na ya kibinafsi ili kupunguza hali ya hatari kwa afya inayotokana na asbestosi.

Asbestosi ni kundi la nyuzi za madini zenye matumizi mengi ya kibiashara ya sasa na ya kihistoria.

Asbestosi, ilitumika sana katika ujenzi nchini Kenya katika miaka ya sitini na sabini, bado imebaki katika majengo ya serikali, hospitali, shule, na hata katika ujenzi wa mifumo ya maji.

“ Imeainishwa kama kansajeni ya binadamu, mfiduo wa asbestosi umeunganishwa kwa hali mbaya kiafya, pamoja na saratani ya mapafu na mesothelioma (saratani ambayo hukuwa kwenye utando wa mapafu, utumbo na moyo),” taarifa kutoka mkutano wa baraza la mawaziri ulioongozwa na rais William Ruto, imesema.

Aina zote za asbestosi zimetathminiwa na shirika la afya Duniani WHO, kuwa husababisha aina kadhaa za saratani na magonjwa sugu ya kupumua.

WHO inasema kwa sababu ya matumizi yake katika vifaa vya ujenzi, mtu yeyote anayehusika katika ujenzi, matengenezo na uharibifu wa majengo ambapo asbestosi imetumiwa ina uwezekano wa hatari, hata miaka mingi au miongo kadhaa baada ya kuwekwa kwa asbestosi hiyo.

Shirika la WHO linasema zaidi ya vifo 200,000 duniani kote kila mwaka, pamoja na mzigo mkubwa wa afya vinatokana na asbestos.

“ Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) itasimamia jukumu hilo la kuondolewa, utupaji na utunzaji wa asbestosi.”mawaziri wameamua.

Serikali za kaunti zilihimizwa kuanzisha maeneo maalum ya kutupa taka zitokanazo na kuondolewa kwa asbestosi.

Chini ya kanuni ya ‘Mchafuzi Hulipa’, wamiliki wa nyumba zenye asbestosi watatakiwa kulima gharama za kuondolewa.

Serikali inatarajia kuwa mpango huu utapunguza siku zijazo mzigo wa magonjwa, kupunguza gharama za huduma za afya, na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us