Mwanaharakati wa Uganda ambaye alikamatwa na kuzuiliwa "bila kujulikana" nchini Tanzania baada ya kujaribu kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani amepatikana ametupwa kwenye mpaka wa Uganda na "dalili za mateso", shirika la kutetea haki za binadamu lilisema Ijumaa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema Tanzania na nchi jirani ya Uganda zimeongeza kasi ya kuwakandamiza wapinzani huku zikijiandaa kwa uchaguzi wa urais katika kipindi cha miezi saba ijayo.
Mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire alikamatwa mapema wiki hii pamoja na mwenzake wa Kenya, Boniface Mwangi, mwanaharakati mashuhuri dhidi ya ufisadi na ukatili wa polisi nchini Kenya.
Atuhaire na Mwangi walikuwa miongoni mwa wanaharakati walioenda Tanzania kuonyesha mshikamano na kiongozi wa upinzani Tundu Lissu wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini Jumatatu.
Amepatikana 'ametupwa'
Lakini Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikashifu kile alichokiita kuingilia masuala ya nchi na kuzitaka idara za usalama "kutoruhusu watu wenye tabia mbaya kutoka mataifa mengine kuvuka mipaka hapa".
Kundi la haki za Uganda la Agora Discourse lilisema kwenye mtandao wa X siku ya Ijumaa kwamba Atuhaire alipatikana "akiwa ametelekezwa mpakani na mamlaka ya Tanzania."
Mwanzilishi mwenza wake Jimmy Spire Ssentongo aliiambia AFP kwamba alikuwa na "dalili za mateso" kwenye mwili wake.
Chama cha Chadema cha Lissu kimepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi wa Tanzania uliopangwa kufanyika Oktoba baada ya kusisitiza kufanyika kwa mageuzi.
Chadema imemtuhumu Rais Samia kwa kurejea kwa mbinu kandamizi za mtangulizi wake, John Magufuli.
Mwanaharakati wa Kenya Mwangi, ambaye pia alipatikana akiwa ametelekezwa kando ya barabara kaskazini mwa Tanzania karibu na mpaka wa Kenya siku ya Alhamisi, kulingana na gazeti la ndani la Daily Nation, alisema walivumilia "mateso ya kutisha".
'Haki zinazoharibika'
Muungano wa makundi ya kutetea haki za binadamu katika kanda umeelezea hatua za hivi punde nchini Tanzania kama "kiashiria cha kuzorota kwa viwango vya haki za binadamu na haki ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki."
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye pia anakabiliwa na mashtaka ya uhaini baada ya kutekwa nyara na watu wenye silaha katikati mwa mji mkuu wa Kenya mwezi Novemba na kuibuka tena siku chache baadaye katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda.
Besigye, 69, amekaa rumande kwa zaidi ya miezi sita -- kikomo cha kisheria kabla ya dhamana ya lazima -- lakini siku ya Ijumaa, mahakama ilikataa kumpa dhamana na kupanga tena kusikilizwa kwake hadi Mei 29.