Kenya, ambayo ndiyo nchi yenye uchumi mkubwa Afrika Mashariki, imekuwa na ukuaji mzuri kila mwaka, lakini deni kubwa la umma, ulipaji mbovu, kutokuwa na usawa katika suala la uchumi na utata kuhusu utawala bora kumefanya hali kuzorota.
"Mikopo ya humu nchini, na riba kubwa kwa mikopo, inapunguza uwekezaji katika sekta binafsi," Naomi Mathenge, mwanauchumi mwandamizi wa Benki ya Dunia, amesema katika ripoti ya tathmini ya uchumi wa Kenya, ambayo huchapishwa mara mbili kwa mwaka.
Serikali imetumia soko la nyumbani kutunisha bajeti yake kutokana na kukosa fedha za kutosha za nje, ripoti hiyo imesema, huku kushindwa kulipa madeni kwa wakati na ukusanyaji mdogo wa mapato kukichangia kuzamisha juhudi za ukuaji.
Mwaka jana mamlaka zilijitahidi kuweka sawa suala la mfumuko wa bei na ubadilishanaji wa sarafu za kigeni, kuruhusu watunga sera kuanza kulegeza masharti, lakini viwango vya riba bado viko juu, ripoti hiyo imesema.
Ukuaji katika sekta binafsi ulikuwa -1.4% Disemba iliopita, Benki ya Dunia ilisema kwenye ripoti yake, ikilinganishwa na ukuaji wa 13.9% mwaka juzi.
Kenya pia inakabiliwa na tatizo la deni lake, ambalo ni 65.5% ya fedha zote zinazokusanywa.
Uchumi ulikuwa kwa 4.7% mwaka jana, kutoka kwa 5.7% mwaka juzi, sababu mojawapo ikiwa ni maandamano ya katikati ya mwaka jana ya kupinga ongezeko la kodi.
Ukuaji unatarajiwa kuimarika hadi 5.0% katika kipindi cha miaka miwili ijayo, Benki ya Dunia imesema.
Benki ya Dunia imetoa wito kwa serikali kutekeleza mabadiliko ya ukusanyaji kodi, ikiwemo kuondoa misamaha ya kodi katika baadhi ya bidhaa, kuongeza ukusanyaji, kuunga mkono juhudi za ukuaji wa uchumi na kupunguza deni.