Jeshi la Uganda limekatiza ushirikiano wote wa kijeshi na Ujerumani baada ya kumshutumu balozi wa Berlin mjini Kampala kwa kuhusika na "shughuli za uasi" katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, msemaji wake alisema.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Jumatatu kuwa shutuma hizo ni "upuuzi na hazina mashiko yoyote na tunazikataa kwa maneno makali".
Msemaji huyo alikataa kuzungumzia zaidi aina ya tuhuma hizo.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda, Chris Magezi, pia hakutoa maelezo zaidi katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye X siku ya Jumapili, mbali na kusema uamuzi huo ulitokana na "ripoti za kuaminika za kijasusi".
Katika chapisho tofauti kwenye jukwaa hilo la X siku ya Jumapili, mkuu wa jeshi la Uganda Muhoozi Kainerugaba alisema jeshi alikuwa na matatizo na Balozi Mathias Schauer "binafsi".
‘‘Inahusiana naye binafsi. Hajahitimu kabisa kuwa Uganda. Haina uhusiano wowote na watu wa Ujerumani," Kainerugaba alisema.