Shirika la Mpango wa Chakula (WFP) lilisema Ijumaa kuwa limefanikiwa kufikia watu milioni 4 pekee nchini Sudan mwezi wa Machi, idadi kubwa zaidi ya watu tangu kuanza kwa vita Aprili 2023, lakini wanaonya kuwa idadi hii bado ni sehemu ndogo ya watu wenye uhitaji mkubwa.
"Hii inajumuisha watu milioni 1.6 katika maeneo ambayo yamewekwa kwenye kundi la njaa kali au katika hatari ya kuwepo kwa njaa kali," amesema Samantha Chattaraj, Mratibu wa masuala ya dharura wa WFP nchini Sudan, wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva.
"Katika mwezi mmoja uliopita, tumesaidia watu wanne kati ya watano wanaokabiliwa na njaa kali katika maeneo 27 ambayo yanakumbwa na njaa au yako kwenye hatari ya kukumbwa na njaa."
Chattaraj ameitaja hali hiyo nchini Sudan kuwa "moja ya hali ngumu sana kwa mashirika ya misaada nchini humo " na kusisitiza kuwa licha ya kupatikana kwa njia ya kufikia watu hivi karibuni, bado mahitaji ni makubwa.
Karibu watu milioni 25, au nusu ya raia wa Sudan, wanakabiliwa na njaa, ikiwemo watoto na kina mama wanaonyonyesha milioni 5 ambao wanakabiliwa na utapiamlo, amesema.
"Sudan pia ni nchi pekee duniani ambapo kwa sasa imethibitika kuwa na njaa kali," alieleza.
WFP inalenga kuwafikia watu milioni 7 kufikia katikati mwa mwaka huu, alisema, wakizingatia zaidi maeneo ambayo hayana chakula cha kutosha.
Hata hivyo, shirika hilo limeonya kuwa uwezo wao wa kuendeleza huduma unategemea msaada wa haraka kutoka kwa wafadhili.
Kwa sasa wanahitaji dola milioni 698 ili waweze kuendelea kutoa misaada kuanzia mwezi Mei hadi Oktoba.
"Kupunguzwa kwa ufadhili huenda kukapunguza kiwango cha chakula kinachotolewa, idadi ya watu watakaopata chakula, na maeneo ambayo misaada itafika," Chattaraj alisema.
"... Kama hatutapata fedha hizi, lengo letu la kuwasadia watu milioni 7 halitotimia."