Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imesema kuwa inao uhalali wa kusikiliza kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ikipiga chini pingamizi la Kigali.
Maamuzi hayo, ya mahakama hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha nchini Tanzania, yanatoa nafasi ya AfCHPR kuanza kusikiliza shauri la ukiukwaji wa haki za kibinadamu katika eneo la Mashariki la DRC.
Katika hukumu yao ya Juni 26, jopo la majaji 11 wa mahakama hiyo, walisisitiza kuwa AfCHPR inao uhalali wa kusikiliza kesi hiyo, wakipinga pingamizi lililowasilishwa na Rwanda, ambayo ilihoji uhalali wa mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.
Ikirejelea vifungu ndani ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, AfCHPR ilisisitiza kuwa ina wajibu wa kusikiliza shauri hilo, na kuitaka serikali ya Rwanda kutuma mawasilisho yao ndani ya siku 90.
Katika usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, Rwanda ilionesha walakini wa shauri la DRC ndani ya mahakama hiyo, ikisisitiza kuwa liliegemea zaidi taarifa za vyombo vya habari, kuliko uhalisia wenyewe.

DRC ilifungua kesi mbele ya AfCHPR mwaka 2023, ikiituhumu Rwanda kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu kufutia mgogoro unaoendelea katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
Katika ombi lake, DRC imeitaka AfCHPR kuishinikiza Rwanda kuondoa vikosi vyake na kuacha kuwaunga mkono wapiganaji wa M23.