Kuna msemo maarufu kwenye lugha ya Kiingereza, wenye kusema, upande mmoja wa ulimwengu ukipiga chafya, basi ule mwingine utaugua ugonjwa wa kifua.
Na ndicho kinachotokea kwa sasa, siku chache baada ya serikali ya Marekani, ikiongozwa na Rais Donald Trump kutangaza vikwazo vya kibiashara kwa mataifa yote duniani, kwa kile anachoeleza kuwa ni kukuza uzalishaji wa ndani wa taifa hilo.
Katika mahojiano yake aliyofanya na waandishi habari Aprili 4, 2025, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Dkt. Yamungu Kayandabila, alisema kuwa japo ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania kuwa mzuri, kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani kunaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuwaji wa uchumi katika kufikia malengo yake.
“Kunapokosekana utulivu katika biashara ikiwemo kubadilika kwa sera za kiuchumi na kibiashara hususani kwa mataifa yaliyoendelea, hata sisi huathirika kiufanisi,” alisema Dkt. Kayandabila.
Maamuzi hayo yameshtua mataifa mengine huku kukiwa na hofu ya kuvurugika kwa mfumo wa uchumi duniani.
Moja ya maeneo ambayo yataathirika na maamuzi haya ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inaundwa na nchi wanachama 8.
Kulingana na ripoti toka kwa jumuiya hiyo, yenye makao makuu yake jijini Arusha nchini Tanzania, kufikia mwaka 2024 mauzo ya bidhaa kutoka EAC yalifikia Dola Bilioni 0.677 huku bidhaa zilizoingia ndani ya jumuiya hiyo ikifikia Dola Bilioni 1.526.
Kanda yenye rasilimali za kutosha
Kanda hiyo iliyojaliwa rasilimali za kutosha, imekuwa ikiuzia Marekani bidhaa mbalimbali kama vile kahawa, majani ya chai, bidhaa za nguo na hata mbogamboga, hususani kupitia mkakati wa Ukuzaji fursa za Kichumi Afrika (AGOA).
“Licha ya AGOA imeturahisishia kwa muda mrefu, kujipenyeza ndani soko la Marekani, mpango huu wa sasa wa Marekani unalenga kufanya bidhaa zetu kukosa ushindani unaotakiwa,” anasema Adrian Njau, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Kuporomoka thamani
Kulingana na Njau, thamani ya ushindani wa bidhaa kutoka Afrika Mashariki itazidi kuporomoka, tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali wakati ushuru ulikuwa ni asilimia sifuri tu.
“Kwa vyovyote vile, mfumo huu mpya utashusha mapato yatokanayo na mauzo ya nje na hivyo kupelekea upungufu mkubwa wa fedha za kigeni, hususani dola ya kimarekani,” anatabainisha.
Hatua hii inaelezwa kuongeza gharama za uendeshaji wa viwanda vya ndani katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Masoko mbadala?
Licha ya sintofahamu hiyo, inayotokana na ushuru huo wa bidhaa, EABC ina amini kuwa lipo suluhisho kwa nchi za EAC kujiepusha au kupunguza makali ya mabadiliko kwenye ushuru wa bidhaa zitakazouzwa nchini Marekani.
“Ipo haja ya kufanya bidhaa zeti ziwe za mseto na kufikiria masomo mapya kama vile bara la Asia,” Njau anaeleza.
Hadi kufikia mwaka 2023, mauzo ya bidhaa za EAC katika soko la bara la Asia yalifikia Dola Bilioni 1.6, wakati ya Mashariki ya kati ilikuwa ni Dola Bilioni 4.7.
“Kwa mfano, kwa sasa, nchi ya China ina mahitaji makubwa ya bidhaa za kilimo kama vile mananasi, maparachichi, korosho na hata mananasi…tukiwa na mazungumzo ya kibiashara na soko hilo jipya, pengine tutaweza kuondokana na kadhia hii,” anashauri.
Hali kadhalika, EABC inasisitiza umuhimu wa nchi za jumuiya ya EAC kuimarisha biashara ya ndani.
Biashara kati ya nchi wanachama wa EAC ilikuwa kwa asilimia 13.1 hadi kufikia Dola Bilioni 12.1 mwaka 2023, kutoka Dola Bilioni 10.6 kwa mwaka 2022, ambacho ni kiashirio cha asilimia 15 ya biashara zote zinazofanyika ndani ya jumuiya ya EAC.
Kujenga ustahimilivu
Kulingana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EABC, kuna haja ya kupunguza utegemezi kwenye masoko ya nje ili kujenga ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya kiuchumi ulimwenguni.
Hii inahusisha kuondoa vikwazo vya biashara na kuoanisha viwango ili kurahisisha na kurahakisha ufanyaji biashara ndani ya EAC, hususani kwa kutumia faida ya uwepo wa itifaki ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).