Polisi nchini Kenya walifunga barabara karibu na sehemu ya kuhifadhi maiti jijini Nairobi huku waandamanaji wakiimba 'Lagat Must Go!'.
Eliud Lagat ni Naibu Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya. Baadhi ya Wakenya wamemnyooshea kidole Lagat ikidaiwa kuwa Ojwang’ alikamatwa kufuatia malalamishi ya naibu huyo aliyemshtumu kwa kumharibia jina kwenye mitandao ya kijamii.
Maandamano hayo yamefuatia kifo cha Albert Ojwang, mwanablogu ambaye alikufa saa chache baada ya kukamatwa na polisi, kwa madai kuwa alihusika katika kusambaza taarifa za kupotosha.
“ Bwana Ojwang sasa anajiunga na orodha ndefu ya vijana wa Kenya ambao wamepoteza maisha yao katika mazingira ya kikatili na ya kutatanisha mikononi mwa polisi,” Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga amesema katika taarifa.
Matokeo ya uchunguzi
Maandamano hayo yalifanyika muda mfupi baada ya uchunguzi wa maiti kufanywa.
"Sababu ya kifo iko wazi sana; jeraha la kichwa, kubanwa kwa shingo na majeraha mengine yameenea mwili mzima ambayo yanaashiria kushambuliwa," Mwanapatholojia wa serikali Bernard Midia alisema.
Uchunguzi wa maiti ya Albert Ojwang ulionyesha kuwa Ojwang’ alikuwa na jeraha kubwa la kichwa.
Pia walihitimisha kuwa majeraha hakujiletea mwenyewe kama vile polisi walivyokuwa wamedai hapo awali katika taarifa yao, na majeraha yake yalionekana hayakutokea tu mara moja.
Kando na majeraha makubwa ya kichwa, wanapatholojia walithibitisha kuwa majeraha mengi ya kichwa, shingo, miguu na mikono na mwili yalisababishwa kutokana na kutumia nguvu.
"Aliteswa vibaya kabla ya kifo chake. Jukumu ni kwa taasisi husika, haswa IPOA, kuhakikisha maafisa waliohusika katika tukio hili wanafikishwa mahakamani, " Hussein Khalid , Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa alisema.
IPOA ni Mamlaka Huru ya Kusimamia utekelezaji majukumu ya Polisi. Inasema imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo chake.
Wakenya wengine wanamtaka naibu mkuu wa polisi ashitakiwe kwa kifo cha Ojwang’.
“Eliud Lagat anatakiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa madai ya mauaji. Kitu kingine chochote hakina msingin ila itakuwa ni kuficha,” Nelson Havi, Wakili maarufu Kenya ameandika kupitia mtandao wa X.
Faith Odhiambo, Rais wa chama cha wanasheria wa Kenya (LSK) anataka polisi wawajibishwe.
“Albert Ojwang’ aliteswa na kuuawa kikatili akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Tunataka kila afisa aliyehusika awajibishwe. Hatutaki visingizio kutoka kwa IPOA.”
Babake Albert Ojwang baada ya matokeo ya uchunguzi wa maiti: alikuwa na maswali haya kwa Naibu Inspekta Jenerali wa polisi,
"Je, wewe ndiwe uliyetuma watu wako? Alifanya nini kustahili haya? Kwa nini mtoto wangu alisulubiwa?" Meshack Ojwang aliuliza.