ULIMWENGU
2 dk kusoma
Iran yaahidi kulipiza kisasi baada ya shambulio la Israeli
Israel imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya mitambo ya nyuklia ya Iran, katika operesheni waliyoiita ‘Rising Lion,’ ambapo baadhi ya viongozi waandamizi wa kijeshi na wanasayansi wa Iran waliuawa.
Iran yaahidi kulipiza kisasi baada ya shambulio la Israeli
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alitoa taarifa yenye maneno makali, akilaani uchokozi huo na kuapa kulipiza kisasi vikali. / AA
13 Juni 2025

Miongoni mwao ni jenerali wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na wanasayansi wanaohusishwa na mpango wa nyuklia.

Licha ya mashambulizi hayo kulaaniwa, Israel imesema yalikuwa ni ya lazima kwa ajili ya kulinda usalama wake wa kitaifa, na kusisitiza kuwa mashambulizi hayo yataendelea kwa siku kadhaa zijazo kwa madai kwamba, Iran inaendeleza mpango wa siri wa kutengeneza silaha za nyuklia kinyume na makubaliano ya kimataifa.

 Iran, kwa upande wake, imelaani mashambulizi hayo na kuituhumu Marekani kwa kushirikiana na Israel katika kupanga na kutekeleza oparesheni hiyo.

Ingawa Marekani imekanusha kuhusika moja kwa moja, lakini imekiri kuwa na taarifa kabla ya mashambulio hayo kufanyika.

Iran imeapa kulipiza kisasi, na tayari kuna ripoti za kuonekana kwa baadhi ya ndege zisizo na rubani katika anga ya Iraq kuelekea Israeli.

Hatua hii imeoongeza wasiwasi wa kuzuka kwa mzozo mkubwa wa kijeshi katika eneo hilo.

 Katika mjadala mpana zaidi, kuna maswali yanayoibuka kuhusu kwa nini mataifa mengine yanaruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia, huku mataifa kama Iran yakizuiwa hata kuwa na teknolojia ya nyuklia.

 Israel yenyewe haijawahi kuthibitisha wala kukanusha kuwa na silaha za nyuklia, lakini haijakumbwa na vikwazo au shinikizo kama Iran.

Hii imesababisha baadhi ya wachambuzi kusema kuwa sheria za kimataifa kuhusu nyuklia zinatekelezwa kwa upendeleo, na zinatumiwa kama chombo cha kisiasa badala ya kuwa mfumo wa haki wa kuhakikisha usalama wa kimataifa.

 Wadadisi wa mambo, tayari wameonyesha hofu ya kuyumba kwa soko la mafuta, iwapo hali hii itaendelea kwa sababu ya athari za usambazaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati, ambayo ni chanzo muhimu cha mafuta kwa duniani.

Wakati huo huo, Marekani bado inatarajia Iran kurudi katika meza ya mazungumzo kujadili mpango wake wa nyuklia.

 

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us