Ugonjwa wa kichaa cha mbwa unavyoathiri Punda nchini Tanzania
AFRIKA
3 dk kusoma
Ugonjwa wa kichaa cha mbwa unavyoathiri Punda nchini TanzaniaKatika halmashauri ya Arusha, matukio ya punda kuonesha tabia zisizo za kawaida ziliwaibua wataalamu wa magonjwa ya wanyama kutoka ASPA.
Idadi ya punda nchini Tanzania inakadiriwa kuwa 600,000, ingawa idadi hii inaweza kutofautiana kutokana na ufugaji na mambo mengine./Picha:ASPA / Others
17 Machi 2025

Katika kikao chao na daktari wa wanyama kutoka halmashauri ya Arusha, wafugaji kutoka kata ya Musa, hawakukubaliana na Daktari wa mifugo kutoka halmshauri hiyo, Linus Prosper kuhusu kile kilichokuwa kinawasibu punda wao.

Wanakijiji hao, ambao hutumia punda kwa shughuli za nyumbani kama vile kubeba kuni na mizigo mingine, waliamini kuwa mifugo yao ilikumbwa na ugonjwa mwingine na sio kichaa cha mbwa, kama walivyoambiwa na Dkt. Prosper.

“Waliamini kuwa nilikuwa nimekosea vipimo, na wakadai kuwa punda hawezi kupata ugonjwa wa kichaa cha mbwa,” anaeleza Dkt. Prosper wakati akitoa mrejesho wake kwa Chama cha Kulinda Wanyama cha Arusha (ASPA).

Idadi ya punda nchini Tanzania inakadiriwa kuwa 600,000, ingawa idadi hii inaweza kutofautiana kutokana na ufugaji na mambo mengine.

Hata hivyo, iko hatarini kupunguza kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa punda.

Katika halmashauri ya Arusha, matukio ya punda kuonesha tabia zisizo za kawaida ziliwaibua wataalamu wa magonjwa ya wanyama kutoka ASPA.

“Tulipata taarifa za baadhi ya punda kuonesha tabia za ajabu kama vile ukali usiokuwa wa kawaida, kujing’ata hata kushambulia na kuwang’ata wanyama wengine,” anasema Lazaro Mirama, daktari wa mifugo kutoka ASPA.

Maambukizi

Kulingana na Dkt. Mirama, punda huachwa ili wajitafutie chakula wenyewe, hali inayowafanya kuwa katika hatari kubwa ya kupata kichaa cha mbwa.

 “Zaidi ya asilimia 90 ya punda hupata ugonjwa wa kichaa cha mbwa kupitia mate ya mbwa mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, na hii hutokea pale punda atakapong’atwa na mbwa mwenye virusi hivyo,” anaeleza Dkt. Mirama katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Hata hivyo, ugonjwa huu sio wa kawaida sana kwa punda, kama ilivyo kwa mbwa, anasema Dkt. Mirama.

Kama ilivyo kwa punda, hata binadamu huugua ugonjwa wa kichaa cha mbwa pale wanapong’atwa na wanyama hao.

Vivyo hivyo, binadamu yupo katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo, iwapo atashambuliwa na kung’atwa na punda.

“Japo kwa punda, itamchukua muda wa wiki moja hadi mbili kwa kupona kwani atakuwa na uwezekano mkubwa wa kufa,” anaeleza.

Udhibiti wa kichaa cha punda

Kwa kushirikiana na Brooke East Afrika, taasisi ya ASPA ilituma wataalamu kwenye maeneo ambayo punda walikuwa wamepata ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Moja ya kaya zilizotembelewa na wataalamu hao, ni pamoja na ile iliyopoteza punda wao kutokana ugonjwa huo.

“Zilichukuliwa sampuli kutoka kwenye mzoga wa punda huyo na kupelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi na majibu yalivyorudi, kweli iligundulika kuwa ni kichaa cha mbwa,” anasema Dkt. Mirama.

Hatua iliyofuata kulingana na Dkt. Mirama ilikuwa ni kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, kabla ya zoezi la kutoa chanjo kwa punda wenye kuonesha dalili za maambukizo kuanza.

ASPA ilitoa chanjo kwa punda wapatao 70 katika kata ya Musa, huku taaisisi hiyo ikiwaasa wakazi wa eneo hilo kuwachanja mbwa wao ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kulingana na Dkt. Mirama, zoezi la kuchanja punda hao lilikuwa ni la umuhimu ili kuepusha wanyama hao kuwang’ata binadamu, iwapo wangepata maambukizi ya kichaa cha mbwa.

Ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa punda uliripotiwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023 ndani ya halmashauri ya Arusha, kabla haujajirudia tena mapema mwaka 2025.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us