Mratibu Msaidizi wa kikundi cha AFC/M23 Bertrand Bisimwa, ameishutumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kutekeleza mauaji ya jamii ya Banyamulenge wanaopatikana maeneo ya Minembe, Uvira na maeneo mengine ya kusini mwa Kivu.
Shutuma hizo zinakuja wiki moja baada ya Bisimwa kudai kuwa vijiji vinavyokaliwa na jamii ya Banyamulenge vilikuwa vikishambuliwa na majeshi ya serikali ya DRC.
Katika chapisho lake kwenye ukurasa wake wa X, Bisimwa alidi kuwa serikali ya Kinshasa ilikuwa ikitekeleza mashambulizi hayo dhidi ya jamii zisizokuwa na hatia, ikisaidiwa na majeshi ya Burundi, wanamgambo wa FDLR kutoka Rwanda na wanamgambo wa Wazalendo.
Siku ya Jumatatu ya Machi 10, kiongozi huyo wa M23 aliweka chapisho lingine kwenye ukurasa wake wa X, akidai kuwa jeshi la DRC lilikuwa likitumia ndege nyuki kupata picha wa jamii ya Banyamulenge.
“Jamii ya eneo ilipata uoga sana. Muda mchache uliopita, wapiganaji wa Sukhoi walipiga mabomu vijiji vya Minembwe,” aliandika.