Akiwa kwenye lindi la mawazo, Mwamvita Ismail ameketi kwenye kiti cha plastiki, ndani ya nyumba yake.
Macho yake ameyaelekeza kwenye sakafu ya nyumba yake iliyojaa maji yaliyopitia kwenye mlango wa nyumba yake.
Pembeni yake, mtoto wake mdogo amesimama akiwa na macho yaliyojaa huzuni na kiu ya kuelewa kwanini hali iko hivi.
Muda wa kwenda madrasa
Kwa kawaida, mtu huyo alipaswa kuwa amekwenda kwenye masomo yake ya madrasa.
Hata hivyo, anashindwa kufanya hivyo kwani barabara katika eneo wanaloishi hazipitiki baada ya kufurika kwa maji yatokayo baharini.
“Maisha yetu yamebadilika sana, kwani hata shughuli zetu za kawaida tunashindwa kufanya,” anasema Mwamvita, mkazi wa eneo la Mikindani mkoani Mtwara.
Onyo la WMO
Kulingana na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO), wastani wa viwango vya vina vya bahari kina cha bahari duniani vimeongezeka kwa kasi zaidi katika karne ya 21 kuliko karne nyingine yoyote katika miaka 3,000 iliyopita.
Wakati huo huo, ongezeko la joto kwenye bahari mbalimbali ulimwenguni, limekuwa kwa kasi zaidi kuliko wakati wowote katika miaka 11,000 iliyopita.
WMO inaonya kuwa, iwapo wastani wa hali joto duniani utapanda kwa nyuzi joto mbili au zaidi, basi viwango vya maji ya bahari vitaongezeka marudufu.
Kuongezeka kwa kina cha bahari au kupanuka kwa bahari ni kitendo kinachotokana na kuongezeka kwa maji baharini ambayo yanasababisha kina cha bahari kuongezeka.
Chanzo cha matokeo haya ya kuogopesha ni mabadiliko ya tabia nchi na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
Jamii zilizoathirika
Wakazi wa kata za Magengeni, Kisungule na Mtonya ni miongoni mwa watu walioathirika zaidi na mabadiliko hayo.
Kulingana na wakazi hao, kabla ya kutokea kwa mabadiliko hayo, Bahari ya Hindi ilikuwa umbali wa zaidi ya mita sitini.
Hata hivyo, kwa sasa, makazi yao yameendelea kumezwa na bahari hiyo.
‘‘Maji chumvi yakiwa yanajaa huwa yanafika mpaka majumbani mwetu, kwahiyo tunapata shida kama tunataka kutoka sehemu moja kwenda nyingine ni changamoto mfano kwenda sokoni, misikitini hata kwenye vituo vya kutolea huduma za afya,” anaeleza Mwanahamisi Sijali.
Changamoto hiyo, pia imeathiri shughuli za uvuvi na kupelekea upatikanaji mdogo wa samaki na viumbe vingine vya bahari ambapo kwa kipindi cha sasa, wavuvi hulazimika kwenda kuvua mbali zaidi, tofauti na zamani, ambapo walifanikiwa kuvua katika maeneo ya karibu na kupata samaki wengi.
‘‘Hali hii imesababisha kuharibika kwa matumbawe na hivyo kuwafanya samaki kusogea kwenye maeneo ya mbali zaidi,” anasema Juma Omary, mvuvi katika eneo hilo.
Kulingana na wakazi wanaoizunguka bahari hiyo, ipo haja ya kupanda miti ya baharini ili kuzuia athari kubwa zinazoweza kujitokeza.
Athari za mabadiliko ya tabia nchi
Kulingana na wataalamu wa masuala ya uhifadhi wa bahari, kina cha bahari huongezeka kutokana na kuyeyuka kwa barafu kunakopelekea ongezeko la joto na mabadiliko katika safu ya bahari ambayo yanatokana na matetemeko ya baharini, volkano, milima, na mabonde.
‘‘Hii sakafu ya bahari ikiwa na vitu kama magugu maji, nyasi bahari na mikoko inasababisha maji kupanda juu, maji yakipanda juu yanaongezeka kwa kuwa yanasukumwa kutoka chini kwenda juu hivyo yanaongezeka upana kutoka sentimita moja kwenda sentimita kadhaa,” anaeleza Paul Mahyige, Mhifadhi Bahari kutoka katika hifadhi ya bahari ya ghuba ya mnazi na maingilio ya mto Ruvuma nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira nchini Tanzania (NEMC) kutoka kanda ya kusini, mhandisi Boniface Guni, changamoto ya kuongezeka kwa kina cha bahari imeathiri kwa kiasi kikubwa maeneo ya mikoa ya Lindi, na Mtwara, na maeneo ya mikoa ya Tanga na Pwani na kupelekea changamoto mbalimbali katika jamii.
‘‘Ni rahisi sana kuona maeneo yaliyopo katika mwambao wa bahari yakiwa yamemegwa,” anasema Guni.
Athari hizo pia zimepelekea kupotea kwa mifumo ya ikolojia ya bahari ambayo imegawanyika katika sehemu tatu; ambazo ni ikolojia ya misitu ya mikoko, matumbawe na nyasi bahari, na pia kusababisha mmonyoko wa ardhi.
‘‘ Tunapata madhara ya kuongezeka kwa mimea au viumbe vamizi kwasababu maji yanapojaa maeneo mbalimbali na kuingia baharini kwa kasi yanaleta viumbe wengine au mimea mingine ambvyo si asili ya eneo husika (baharini),” anasema Mahyige.
Athari kiuchumi
Mabadiliko haya pia yamesababisha kupotea kwa maeneo ya uwekezaji, uharibifu wa miundominu na kutoweka kwa furza za kitalii.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, serikali ya Tanzania imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani 742,115, kulingana na Afisa Maliasili na Mazingira mkoani Mtwara, Ronald Pangha.
Fedha hizo zitatumika kujenga kujenga ukuta na kuweka matuta zaidi ya 13 kwa ajili ya kuzuia kupanuka kwa bahari, na kutengeneza eneo la fukwe ili kukabiliana na changamoto hiyo, huku jitihada zingine za kutoa elimu zikiendelea kwa jamii.