Mawigi yapigwa marufuku katika mashindano ya urembo Côte d'Ivoire
Mawigi yapigwa marufuku katika mashindano ya urembo Côte d'Ivoire
Waandaji wa mashindano ya Miss Côte d'Ivoire wamepiga marufuku washiriki kuvaa mawigi na kuongeza nywele za bandia ili kusisitiza "urembo asili wa Kiafrika", jambo lililozua mjadala mkubwa.
5 Machi 2025

Na Pauline Odhiambo

Zaidi ya miaka 5,000 iliyopita,mawigi na nywele zingine bandia yalikuwa maarufu miongoni mwa watu wa tabaka la juu nchini Misri, nchi asili ya nywele bandia. Tafakari kuhusu mafarao, malkia na watu wa tabaka la juu.

Kipindi cha biashara za utumwa, hali ilibadilika. Wanawake watumwa walilazimishwa kuvaa mawigi ili muonekano wao uwe kama watu wa magharibi, mtindo ambao ulianza kuwa maarufu kwa jamii ya watu wenye asili ya Kiafrika kote duniani.

Sasa, wanawake wenye asili ya Kiafrika ni miongoni mwa kundi kubwa linalotumia mawigi na nywele za nyongeza kote duniani.

GlobeNewswire, shirika linaloshughulika na usambazaji wa masuala ya taarifa, limeripoti kuwa 50% ya wanawake wa Kiafrika wanavaa nywele bandia, huku wengine wengi wakivaa mawigi kulinda nywele zao asili zisiharibike, hasa kama nywele zenyewe ni kavu.

Nigeria na Afrika Kusini ndiyo mataifa yenye wateja wengi wa nywele bandia na mawigi barani Afrika. Kulingana na data kutoka jukwaa la Business Market Insights, thamani ya bidhaa hiyo kwenye soko la bara Afrika ni dola milioni $272 mwaka 2022, na inatarajiwa kuongezeka hadi dola milioni $412.53 kufikia 2030.

Mtazamo mpya

Kwa muda mrefu mawigi na nywele bandia yamekuwa yakipendwa katika sekta ya urembo, kufanya iwe rahisi kwa mtu kupendeza na kuenda na mtindo wowote.

Hasa katika mashindano ya urembo, ambapo unapata watu wakichagua mawigi marefu ili waonekane kama wazungu wenye nywele ndefu na zilizonyooka.

Marufuku ya hivi karibuni kwa washiriki wa mashindano ya urembo ya Miss Côte d'Ivoire yamesababisha watu kuanza kutafakari upya.

Tarehe 28 Januari, waandaaji waliamua kubadilisha hali ya mambo kwa kutaka watu wawe na nywele zao za asili, ziwe ndefu, fupi, zimesukwa au kunyolewa.

Wakati wakisisitiza umuhimu wa kufurahia urembo asili wa Kiafrika na uhalisia, rais wa kamati ya Miss Côte d'Ivoire, Victor Yapobi, alieleza kuhusu washindi wa zamani wa mashindano ya urembo ya dunia ambao walikuwa na nywele fupi za asili.

"Wote wanaotaka kushiriki mashindano ya Miss Côte d'Ivoire lazima waje wakiwa na nywele zao za asili," Yapobi alisema mjini Abidjan kabla ya makala ya 29 ya mashindano hayo ya urembo.

"Mabadiliko haya yanatokana na vile watu wanahoji kuhusu kuwa na mawigi na nywele zingine bandia, ambazo mitindo yake na muundo si sehemu ya utamaduni wa watu wa Cote d’Ivoire."

Masharti hayo mapya yalihamasishwa na Marlene Kouassi, mshindi wa Miss Cote d’Ivoire 2022. Alishiriki katika mashindano ya urembo akiwa na nywele fupi.

Kujikubali

Hatua hii inalenga kuwafanya wanawake wajiamini na kujikubali kama walivyo bila ya kuongeza vitu bandia.

Yapobi alisema kuwa sheria mpya za mashindano ya urembo zinalenga kuhakikisha kuwa washiriki wanajiamini na kujikubali, pamoja na kuwahamasisha wanawake wengi zaidi kutambua nywele zao asili.

Pamoja na kuwa baadhi ya watu wanasema ni hatua nzuri, mwanasosholojia Gnelbin Nicaise Hlil anaamini mabadiliko haya yanachukuwa muda kwa ndoto kutimizwa.

"Hatua hii ya kuwapa watu fursa ya kujitambua na kufahamu nywele zao asili imeanza kitambo. Na tukiangalia jamii kwa makini, tunaona kuwa baadhi ya mambo yanapungua. Bado watu wanapaka mkorogo, pia bado watu wanavaa mawigi," anasema Hlil.

Hisia tofauti

Uamuzi wa kupiga marufuku mawigi na nywele za ziada kwenye mashindano ya urembo ya Miss Côte d'Ivoire wengi wameutaja kuwa wa "kihistoria", licha ya kuwa wengine wanahoji kuwa huku ni kuingilia uhuru wa mtu binafsi.

"Côte d'Ivoire imeanzisha hili na naamini nchi zingine zitafwata hivi karibuni," Mkenya Linda Karanja, ambaye hufwatilia kwa karibu mashindano ya urembo ya dunia, ameiambia TRT Afrika.

Marguerite Koutouan, msusi mjini Abidjan, anasema kutovaa mawigi pia kunamfanya mtu asiweze kupata madhara kwenye kichwa chake.

"Baadhi ya mawigi yanasababisha mtu kupoteza nywele au kuwa na tatizo lisilotibika kwenye kichwa kwa sababu ya kuweka wigi kimakosa au kuweka gundi vibaya. Sasa, warembo wetu wanaweza kuwa na nywele zao za asili na wasiwe na hofu ya kupoteza nywele ," anafafanua.

Mfanyabiashara wa Nigeria Karim Aboubakar anaona bora washiriki wa mashindano ya urembo wawe na maamuzi ya namna wanavyotaka nywele zao zionekane.

"Wakati mwingine mitindo ya nywele ni chaguo la mtu, asillazimishwe. Uwe mshiriki wa kizungu, kutoka bara Asia au Latino vaa wigi na nywele za kuongeza, kwa hiyo suala la kumnyima mtu uhuru wa kuchagua anachotaka ni kukandamiza wanawake wenye asili ya Kiafrika," anaiambia TRT Afrika.

Baadhi ya mabadiliko kwa sheria za washiriki wa mashindano ya urembo ya Côte d'Ivoire ni masharti kuhusu kimo cha mshiriki, ambapo sasa kimepunguzwa kutoka 1.68m hadi 1.67m. Na umri wa juu wa kushiriki umebadilika kutoka kwa miaka 25 hadi 28.

Mchujo wa awali wa washiriki wa Miss Côte d'Ivoire 2025 utafanyika hadi tarehe 10 Mei, huku mshindi akitarajiwa kutangazwa tarehe 26 Juni.

 

Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us