Shirika la Maendeleo ya Nishati nchini Rwanda (EDCL) kimesema kuwa ujenzi wa kiwanda kipya cha kuzalisha umeme kwa maji cha Nyabarongo II, unaendelea kwa matarajio.
Huu ni mradi mpya zaidi wa kuzalisha umeme kwa maji nchini Rwanda.
"Tunafuatilia maendeleo kila siku. Tumekamilisha karibu asilimia 50 ya kazi na tunatarajia maendeleo mengi zaidi ifikapo mwisho wa mwaka," Mkurugenzi Mkuu wa EDCL Felix Gakuba alisema wakati wa kikao cha Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni.
Alisema vipengele muhimu vya miundombinu tayari vinatengenezwa.
Serikali ya Rwanda inasema bwawa hilo la megawati 43.5 katika Mto Nyabarongo limeundwa sio tu kuzalisha umeme lakini pia kusaidia umwagiliaji maji katika zaidi ya hekta 20,000 za mashamba, kusambaza maji, na kupunguza mafuriko katika maeneo ya chini ya mto.
Mradi huo ulianzishwa kufuatia makubaliano ya mfumo wa Februari 2020 kati ya serikali ya Rwanda na China, ambapo Benki ya Exim ya China inatoa mkopo wa masharti nafuu wa $214 milioni kufadhili ujenzi.
Mkurugenzi Mkuu wa EDCL Felix Gakuba alibainisha hasa kuwa muundo wa kituo cha umeme ( powerhouse) umefikia kiwango chake cha kwanza, na msingi wa bwawa umekamilika.
Amesema sasa umakini uko kwenye sehemu za juu za bwawa, ambazo zinatarajiwa kuchukua miezi minne hadi mitano kujengwa kabla ya viwango zaidi kuongezwa baada ya kuimarishwa kwa muundo.
Gakuba pia alisema ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme umeanza, huku wakandarasi wakiwa tayari wapo kazini.
Aidha, vifaa vya mitambo ya kuzalisha umeme ambavyo vingi vimetengenezwa nchini China viko njiani kuelekea Rwanda.
"Wafanyakazi wetu walisafiri hadi China kukagua vifaa kabla ya kusafirishwa," aliongeza.