Tetemeko lenye ukubwa wa 6.2 limepiga Uturuki, huku kitovu kikiwa wilaya ya Silivri iliyopo Istanbul, kwa mujibu wa Kitengo cha Maafa na Dharura cha Uturuki (AFAD).
Tetemeko hilo limepiga majira ya saa 6:49 muda wa Istanbul na kusikika zaidi Istanbul siku ya Jumatano na mikoa jirani, hivyo kusababisha wakazi kutoka majumbani kwa hofu.
Tetemeko jengine lenye ukubwa wa 4.9 limepiga saa 7.02 mchana, huku likisikika zaidi katika pwani ya Buyukcekmece katika Bahari ya Marmara.
AFAD imesema taasisi husika ziko katika tahadhari na tathmini inafanyika kubaini uharibifu na kuhakikisha usalama wa raia.
AFAD imesisitiza kuwa vikosi vinafuatilia na kuratibu jitihada za mwitikio.
Mpaka sasa hakuna taarifa za madhara au uharibifu mkubwa.
Katika taarifa, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema mamlaka inafuatilia kwa karibu yanayojiri.