Inaaminika kuwa alizaliwa akiwa na umbo kubwa, na hivyo mama yake kumpa jina la Kidum au Kidumu, yaani gudulia kubwa la kuhifadhia vimiminika, ila jina lake halisi ni Jean-Pierre Nimbona.
Mzaliwa wa nchini Burundi, miaka 50 iliyopita, Kidum alianza kuonesha mapenzi yake kwenye sanaa ya muziki akiwa na umri wa miaka 10 tu, kwa kupiga ngoma.
Alianzisha kundi lake mwenyewe ambalo lilianza kupiga muziki nchini Burundi, lakini halikudumu kwa muda mrefu kufuatia kuibuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1993.
Katika mahojiano yake na jarida moja nchini Kenya miaka sita iliyopita, Kidum ambaye aliachia albamu zilizompa maarufu kama vile Yaramenje (2001), Shamba (2003)Ishano (2006), Haturudi Nyuma (2010) na Hali na Mali ya mwaka 2012, anasimulia namna alivyokuwa akilazimika kukimbilia nchini DRC, kukwepa vita nchini Burundi, kati ya mwaka 1993 na 2005.
Njia panda
Kidum anakumbuka alivyojikuta njia panda, hasa ukizingatia kuwa mama yake alikuwa ni Mhutu, huku baba yake akitokea jamii ya Kitutsi, wakati vita hivyo vikiwa vimepamba moto nchini Burundi.
Kidum anakumbuka namna vijana wa rika lake walivyolazimika kuingia jeshini ili kutetea jamii zao, na yeye kuamua kukimbilia nchini DRC kabla ya kurudi tena Burundi kuendelea na masomo yake.
Kidum anasimulia mkasa wa kusikitisha uliowakuta wanafunzi wenzake 17, ambao alikuwa amepanga nao kwenda kutembelea shule ya wasichana iliyokuwa jirani.
Kwa mujibu wa Kidum, wote kwa pamoja walikubaliana waamshane, ila kwa bahati mbaya, wanafunzi wenzake hawakufanya hivyo, na hivyo kuamua kwenda peke yao.
Hata hivyo, wanafunzi hao waliuwawa na wanajeshi msituni kabla ya kufika mwisho wa safari yao.
Kukimbia vita
Hali hiyo ilizidi kumtia hofu Kidum, ambapo baba yake alilazimika kumpa dola 60 za Kimarekani ili akimbie machafuko hayo na kwenda kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanamuziki.
Kidum anakumbuka namna alivyovuka mpaka na kuingia nchini Tanzania, na kulazimika kutafuta hifadhi chini ya madaraja na misikitini, kabla kujilipia usafiri na kuelekea jijini Nairobi nchini Kenya na baadaye katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma.
Baada ya kifo cha baba yake, Kidum aliamua kuhamia Kenya mazima.
Kidum, ambaye ameoa mke kutoka eneo la Bungoma nchini Kenya amejaliwa kupata watoto saba, japo kwa wanawake tofauti.
Anamiliki bendi yake iitwayo ‘Bodaboda band ambayo iliwahi kwenye‘Churchill Show’ nchini Kenya.
Ushirikiano na wasanii
Amewahi kushirikiana na wanamuziki mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki, akiwemo Lady Jay Dee kupitia wimbo wa ‘Nitafanya’, Haturudi Nyuma aliyorekodi na Juliana Kanyomozi na wimbo ‘Relax’ aliouimba na Peter Msechu.
Kidum ni mshindi wa tuzo ya Pearl Music Awards, Kora Music Awards, ISC Music Award na Buja Music Awards.