AFRIKA
2 dk kusoma
Gachagua akanusha madai ya kupanga njama kupindua serikali kwa maandamano Kenya
Naibu huyo wa Rais wa zamani amekana kuhusika na makundi ya wahalifu waliovuruga maandamano nchini Kenya na kusema kama kweli kuna ushahidi dhidi yake, mbona hajatiwa nguvuni hadi sasa?
Gachagua akanusha madai ya kupanga njama kupindua serikali kwa maandamano Kenya
Rigathi Gachagua, Naibu rais wa zamani amekua akizozana na serikali ya WIlliam Ruto tangu alipoondolewa ofisini /Picha:reuters
28 Juni 2025

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amepuuzilia mbali madai kwamba alifadhili au kuandaa makundi yaliyovuruga maandamano ya Juni 25 nchini Kenya na kusababisha ghasia.

Gachagua aliuliza kama kweli kun aushahidi dhidi yake, kwanini hadi sasa hajakamatwa na polisi au hata kutakiwa kwa ajili ya upelelezi?

"Ikiwa kweli nilifadhili wahuni, ikiwa ninahusika na machafuko hayo, kwa nini hawajanikamata?" aliuliza. "Kama kulikuwa na taarifa za kijasusi kwamba Gachagua alifadhili majambazi, polisi wanangoja nini? Nikamateni!"

Isitoshe, Gachagua, ambaye alikuwa akizungumza katika mahojiano kwa televisheni, alitaja madai hayo kama uchafuzi wa kisiasa unaolenga kuchafua jina lake na njama ya kufumba wananchi macho juu ya kushindwa kwa serikali.

Machafuko yaliyojificha kama dekorasia

Kauli yake ilikuja saa chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen kutaja maandamano yaliyoongozwa na Gen Z kama "jaribio la mapinduzi," akidai kuwa maandamano hayo yalikuwa na ufadhili wa kutosha, operesheni ya kisiasa inayolenga kupindua serikali.

Murkomen alidai kuwa waandamanaji walilenga vituo muhimu vya serikali ikiwa ni pamoja na Bunge, Ikulu na vituo vya polisi, akiongeza kuwa kulikuwa na ushahidi wa uratibu na mipango ambao uliashiria uchochezi wa hali ya juu.

Rais William Ruto, katika hotuba yake ya Alhamisi, alikashifu ghasia hizo, na kuzitaja kama "machafuko yaliyojificha kama demokrasia" na kuwaagiza polisi kuwatambua na kuwashtaki wanaopanga mipango na wafadhili. Pia alionya kuwa kutafuta mamlaka kupitia ghasia badala ya uchaguzi hakutavumiliwa.

Maandamano ya Juni 25 yalilenga kuwa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kufanywa maandamano ya Gen Z yaliyopinga mswada wa fedha n akumlazimu Rais Ruto kufanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri.

Vifo na majeraha

Hata hivyo muda mfupi baada ya kuanza ghasia ziliibuka huku makundi ya wahuni waliojihami wakivamia maduka na kuchoma moto mali za watu.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeweka idadi ya waliofariki kutokana na maandamano ya Jumatano kuwa 16, huku zaidi ya 400 wakijeruhiwa - wengi wao kutokana na kupigwa risasi na polisi.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us