Mahujaji wanapokuwa katika ibada hiyo, baadhi hukutwa na mauti wakiwa huko, na hii husababishwa na mambo kadhaa, ikiwemo msongamano wa watu, shinikizo la damu na presha kutokana na mabadiliko ya hali hewa, lakini pia umri na sababu nyengine za kiafya.
Kutokana na sababu hizo, ndio maana baadhi kabla ya kuondoka nchini, huamua kuacha wosia kwamba iwapo wameaga dunia wakiwa katika ibada hiyo, basi wazikwe huko huko bila kusafirishwa.
Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu, ardhi ya Makkah na Madina ndio ardhi tukufu zaidi duniani, ambayo historia yake ilianzia kwa Nabii Ibrahim, alidiriki kuiombea Amani na utulivu ardhi hiyo.
Hivyo, kwa Muislamu, kufa na kuzikwa huko, ni sawa na kupata makazi yake mazuri katika eneo hilo, basi ni fahari kubwa, na hasa iwapo kifo kimemkuta akiwa katika ibada ya hijja, basi inakuwa ni ishara njema.
Mbali na Makkah kwamba ndipo alipozaliwa Mtume Muhammad Rehema na Amani Zimfikie, Madina napo ndipo alipozikwa yeye na baadhi ya Maswahaba wake, hivyo kwa Muislamu, nae ubavu wake kulazwa katika ardhi aliyozikwa Mtume Rehema na Amani Zimfikie, bado inakuwa ni fahari kubwa kwake, na kwa ndugu zake.
Hivyo basi, kwa Waislamu, mtu kufa na kuzikwa katika maeneo hayo, sio jambo la kujutia, bali kwa wengine, ni ndoto ya muda mrefu iliyoambatana na maombi.