Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, amerekodi taarifa rasmi mbele ya Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) leo, tarehe 19 Juni, kuhusiana na kifo cha mwanablogu Albert Ojwang’ aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi.
Kabla ya tukio hilo, Lagat alikuwa amewasilisha malalamiko dhidi ya Ojwang’, akimtuhumu kwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii.
Na hivyo kusababisha kukamatwa kwa mwanablogu huyo kutoka nyumbani kwake katika Kaunti ya Homa Bay na kupelekwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi jijini Nairobi, ambako alifariki akiwa rumande saa chache baada ya kutiwa nguvuni.
IPOA imethibitisha kuwa maafisa wa polisi zaidi ya ishirini tayari wamehojiwa na kurekodi taarifa kuhusiana na tukio hilo.
Kifo cha Ojwang’, ambacho kimeibua maswali mengi na kuzua hisia kali kote nchini, kimechochea wito wa hatua kali dhidi ya wahusika wakuu ndani ya idara ya polisi.
Shinikizo la kitaifa limekuwa kubwa kiasi cha kulazimisha Eliud Lagat kujiuzulu kutoka wadhifa wake siku ya Jumatatu, hatua ambayo IPOA imetaja kuwa muhimu kwa ajili ya uchunguzi huru usio na ushawishi wa mamlaka yoyote.
Uchunguzi rasmi unaendelea, huku IPOA ikijitahidi kubaini ukweli wa kilichotokea hadi kusababisha kifo cha mwanablogu huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi.