Wakenya wanatarajiwa kuandamana kwa wingi barabarani siku ya Jumatano kuadhimisha mwaka mmoja wa maandamano ya kuipinga serikali ambayo yalifikia kilele kwa kushambuliwa kwa bunge na vifo kadhaa huku polisi wakiwafyatulia risasi waandamanaji.
Makundi yalionekana kukusanyika pembezoni mwa jiji la Nairobi, huku baadhi wakianza kutiririka kuelekea kati kati mwa jiji.
Maandamano haya yanalenga kumulika ukatili wa polisi hasa katika kukabiliana na waandamanaji ambapo polisi wameshutumiwa kuwapiga risasi na hata kuwaua baadhi ya waandamanaji huku wengine wakisemekana kuuawa wakiwa kizuizini.
Maandamano haya tayari yamezua hofu ya kutokea mapambano makali, baada ya msemaji wa polisi Isaac mwaura kutangaza siku mbili zilizopita kuwa maandamano ayo hayakuwa halali, licha ya waandamanaji kuwasilisha mapema notisi kwa polisi.
Rais William Ruto pia amesema anasimama na vyombo vy ausalama katika hili na kusisitiza umuhimu wa kulinda maisha na mali za raia.
Kutokana na hofu ya fujo na uharibifu, wafanya biashara jijini Nairobi wameziba madirisha yao na kuondoa bidhaa zao kwa uhifadhi.
wakati huo huo video zimesambazwa mitandaoni za Gen Z wakihimizana kutokea kwa wingi kushiriki maandamano wanayosema ni ya amani.