Jeshi la DRC limetangaza kuidhibiti ndege isiyokuwa na usajili iliyokuwa imeingia kwenye anga la nchi hiyo.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi hilo Sylvain Ekenge, amenukuliwa akisema kuwa ndege hiyo ilikuwa inaelekea katika eneo la Kivu Kusini bila kupewa ruhusa kutoka mamlaka ya usalama wa anga nchini humo.
Kulingana na taarifa hiyo, jeshi la nchi hiyo “lilichukua maamuzi madhubuti” ya kulinda usalama wa DRC.
Siku ya Jumatatu, waasi wa M23 waliishutumu serikali ya DRC kwa kulipua ndege ya kiraia iliyokuwa imebebab misaada ya kibinadamu, kuelekea katika eneo la Minembwe, Kusini mwa jimbo la Kivu.
Msemaji wa kikundi hicho, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa shambulio hilo liliharibu misaada muhimu ya kibinadamu, ikiwemo madawa na vyakula.
Waasi hao wameendelea kuituhumu serikali ya DRC kwa kukiuka makubaliano ya usitishwaji wa machafuko, katika eneo la Mashariki la nchi hiyo.
Tukio hilo linakuja siku chache baada ya serikali ya DRC na ile ya Rwanda, kutiliana saini mkataba wa amani jijini Washington nchini Marekani, wenye nia ya kumaliza mgogoro katika eneo la Mashariki mwa DRC.