Wizara ya Afya ya Rwanda imesema inajiandaa kuzindua mpango mpya wa kutoa huduma za matibabu kwa watu.
Inafanya majaribio ya huduma ya afya kupitia kituo kipya kitakachoruhusu wataalamu wa matibabu kushauriana na kuwatibu wagonjwa kutoka maeneo mbali mbali ya nchi.
Wataalamu hao watakuwa na makao yao katikati mwa jiji la Kigali lakini wataweza kusaidia wagonjwa na watoa huduma za afya katika hospitali na zahanati kote nchini bila kuhitaji kuwepo eneo la tukio.
Hospitali hiyo itatumia teknolojia maarufu kama ‘telemedicine,’ mbinu inayotumia teknolojia ya kidijitali kama vile simu za video, programu za simu na majukwaa ya mtandaoni kutoa huduma za afya kwa mbali.
Muhammad Semakula, Mkuu wa Idara ya Mipango, Ufuatiliaji, Tathmini na Ufadhili wa Afya katika Wizara ya Afya, alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Rwanda wa kukabiliana na uhaba wa madaktari na wataalamu nchini.
"Tunaamini kwa hiyo tunaweza kutoa huduma nyingi na tunaweza kupunguza hatari ya kupoteza maisha," alibainisha.
Alieleza kuwa walitengeneza zana za matibabu ya teknolojia kusaidia madaktari katika kuungana na wagonjwa katika hospitali za wilaya.
Kwa kutumia modeli za hisabati, mfumo unaweza kutathmini kila mgonjwa anapofika katika kituo cha afya na kuainisha kama wapo katika hatari kubwa au ndogo.
Mgonjwa akitambuliwa kuwa katika hatari kubwa, atapokelewa mara moja katika kituo cha afya lakini pia kupitia jukwaa la teknolojia.
"Tutakuwa na madaktari wawili wa magonjwa ya wanawake wanaotoa huduma kwa hospitali 10 za wilaya ambazo zina viwango vya juu vya vifo vya uzazi," Semakula aliongezea.
"Iwapo majaribio yatafanikiwa, tutapanua mradi ili kuunda hospitali hizo za teknolojia ambazo zitatoa huduma nyingi zaidi, ikiwa ni pamoja na idara mbalimbali zilizo na taaluma tofauti."