Watumiaji wa nishati hiyo nchini Tanzania wanaendelea kushuhudia ongezeko la bei ya petroli licha ya kushuka kwa bei katika soko la kimataifa.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (EWURA) imetangaza ongezeko la bei ya nishati ya petrol kwa watumiaji wa rejareja wa huduma hiyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa Aprili 2, 2025, EWURA, wakazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa gharama ya Dola za Kimarekani 1.14(Shilingi 3,037 za Kitanzania) kutoka Dola 1.13( Shilingi 2,996 za Kitanzania) mwezi uliopita.
EWURA imesisitiza kuwa, bei kikomo za mafuta kwa mwezi Aprili zimepungua kwa asilimia 6.92 kwa mafuta ya petroli, asilimia 6.57 kwa dizeli na asilimia 7.82 kwa mafuta ya taa.
Katika taarifa yake, mamlaka hiyo imesisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petrol zitaendelea kupangwa na soko.
“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mamlaka hiyo pia imebainisha kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa bei hizo zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA.