Mazungumzo kati ya DRC na M23 yanaashiria nini?
AFRIKA
4 dk kusoma
Mazungumzo kati ya DRC na M23 yanaashiria nini?Haijafahamika mara moja, iwapo serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), itakuwa tayari kwa majadiliano hayo, ikiwa imeshakataa fursa hiyo mara kadhaa hapo nyuma.
M23 sasa inadhibiti maeneo yote ya kibiashara nchini DRC yanayoelekea mpaka wa Rwanda, Februari 27, 2025 (REUTERS/Victoire Mukenge)
12 Machi 2025

Raia wa DRC wameishi katika hofu kubwa, tangu kuanza kwa mwaka 2025.

Hii ni baada ya waasi wa M23, moja ya vikundi vyenye silaha nchini humo, kufanya mashambulizi katika eneo la Kivu, na kuuteka mji mkuu wa Goma, Kivu Kaskazini na baadaye kudhibiti eneo la Kivu Kusini.

Jitahada zisizoisha za kulitaka kundi la M23 kusitisha vita hivyo, bado hazijazaa matunda.

Angola, ambaye ni mjumbe wa amani ndani ya Umoja wa Afrika imesema kuwa itajaribu kufainasema kuwa itajaribu kufanya mazungumzo ya ana kwa ana, yatakayohusisha waasi wa M23 na DRC.

"Angola, kama mpatanishi katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, itaanzisha mawasiliano na M23, ili wajumbe kutoka Congo na M23 wafanye mazungumzo ya moja kwa moja huko Luanda siku chache zijazo," taarifa kutoka ofisi ya Rais wa Angola ilisema.

Hata hivyo, haijabanika wazi ikiwa serikali ya DRC, ambayo imekataa mara kwa mara kufanya mazungumzo na M23, itashiriki majadiliano hayo.

"Mazungumzo na kikundi cha kigaidi kama M23 ni mstari mwekundu ambao hatutawahi kuuvuka." Rais Felix Tshisekedi alisema Januari 2025.

Hata hivyo, kwa wakati huu, serikali ya DRC inasema kuwa bado inazingatia jitihada za Angola kuleta amani katika eneo la Mashariki mwa DRC.

“ Tunazingatia na kusubiri kuona utekelezaji wa mchakato huu wa upatanishi wa Angola. Pia tunakumbuka kwamba kuna mfumo ulioanzishwa awali ambao ni mchakato wa Nairobi na tunathibitisha tena utayari wetu kwa azimio hilo.”

Katika mkutano wao Februari 8, 2025, viongozi na wakuu wa nchi kutoka ukanda wa EAC na ule wa SADC, waliitaka DRC ikutane ana kwa ana na kikundi cha M23.

M23 itaondoka mashariki mwa DRC ?

Bado haujulikani iwapo mazungumzo hayo yatashawishi kikundi cha M23 kuondoka katika maeneo ambayo inaendelea kuyashikilia.

Umoja wa Mataifa unaonya kuwa hali ya usalama inazidi kuzorota nchini DRC.

“ Hali ya usalama wa kibinadamu nchini DRC inaendelea kuzorota huku mamia kwa maelfu ya watu wakihama katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini. Takriban watu 80,000 wamekimbia mapigano na kuingia nchi jirani, wakiwemo watu wapatao 61,000 ambao wamewasili Burundi tangu Januari mwaka huu,” lilisema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

“ Katika wiki mbili za kwanza za Februari, matendo ya ubakaji yapatayo 895, ambayo ni sawa na wastani wa matukio 60 kwa siku, yaliripotiwa,” shirika hilo limeongeza.

Kwa upande mwingine, sekta ya kilimo imezidi kuathirika huku watu wengi wakiishi kwa hofu baada ya kutoroka kwa maofisa wa usalama nchini DRC na wengine kukamatwa na kulazimishwa kujiunga na M23.

Majadiliano hayo lazima yaihusishe Rwanda.

Shinikizo la kimataifa linaonekana kuongezeka kwa kasi dhidi ya M23 na Rwanda, ambayo inashutumiwa kuunga mkono kundi hilo.

Rwanda inaendelea kukana hayo huku Rais Paul Kagame akisema uamuzi wa kupata amani lazima ufanywe na Wacongo wenyewe.

“ Sasa kinachohoitajika ni kwa washikadau wanaohusika na wale wanaotaka kuunga mkono jitihada ya amani kusitisha vita,” alisema Rais Paul Kagame wa Rwanda katika mahojiano yake hivi karibuni.

“ Pili ni kutafuta mchakato unaotatua shida za kisiasa kwa amani , hii itahitaji viongozi wa DRC kuchukua hatua na kusema ‘nitaongea na wacongo wanaonipinga na kusikiliza wanahitaji nini’. Hata kama wataamua kati ya mahitaji 10 wachukue sita tu, hayo ndiyo maendeleo,” aliongeza Rais Kagame.

Rwanda inasisitiza kuwa imechukua hatua ya kulinda mipaka yake dhidi ya kuingiliwa na DRC.

Amesema pia ni lazima serikali ya DRC kutoa suluhu kwa changamoto dhidi ya Rwanda iliyo na mizizi nchini humo, akimaanisha kikundi cha FDLR.

FDLR ni mojawapo ya makundi ya mwisho ya waasi wa Rwanda wanaoishi nchini DRC. Kilianzishwa mwezi Septemba 2000, kupitia muungano wa makundi mengine ya wakimbizi wa Rwanda.

Mashambulizi mapya ya M23 nchini DRC yamechochea uhasama kati ya viongozi wa nchi hizo mbili. Kulingana na Rais Paul Kagame, mara ya mwisho kwake kufanya mazungumzo na Rais Tshisekedi ilikuwa ni mwaka 2022.

Vikwazo kwa Rwanda

Mnamo Februari 20, 2025, Marekani ilimuwekea vikwazo James Kabarebe, ambaye ni Waziri wa Nchi wa Rwanda anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, na Lawrence Kanyuka Kingston, msemaji wa M23, pamoja na kampuni mbili za Kanyuka zilizosajiliwa nchini Ufaransa na Uingereza.

Uingereza, Canada na Ujerumani pia zilitangaza hatua mbalimbali Februari 25, 2025, Machi 3 na Machi 4 mtawalia, ambazo ni pamoja na kuzuia au kusimamisha misaada ya kifedha ya nchi mbili na ushirikiano wa maendeleo na Rwanda.

Kigali imekosoa maamuzi haya, ikisema kuwa hatua hizo hazitasaidia kutatua hali ya mashariki mwa DRC.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us