Katika kuonesha umahiri wa sanaa na kuibua vipaji, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ain Shams,katika mji mkuu wa Misri, Cairo wameandaa tamthilia inayoangazia suala la uhamiaji haramu na changamoto wanazopitia watu wanapokuwa mataifa ya magharibi.
Tamthilia hii ni sehemu ya mradi wa chuo hicho kwa wanafunzi wanaojifunza lugha ya Kiswahili, mhadhiri wao Shaimaa Tarek akiwa msimamizi wa zoezi hilo.
‘’Nilikuwa na wazo hili kwa kipindi cha miaka mitatu, mimi ninapenda uigizaji sana na nilitamani kufanya tamthilia ya Kiswahili. Kwa hiyo nimekuwa na wazo hili kwa muda mrefu.’’ Bi Tarek anaeleza namna fikra hiyo ilipoanza.
Lengo kuu anasema ni kukuza lugha ya Kiswahili, ‘’Kitu kilichonihamasisha ni nia ya kuimarisha lugha ya Kiswahili hapa Misri na Duniani kote, pia hakujakuwa na tamthilia kwa lugha ya Kiswahili iliyofanywa nchini Misri kwa hivyo niliamua kufanya kitu cha tofauti’’, aliongeza Shaimaa.
Tamthilia hii ya ``Ndoto Bandia’’ ina sehemu nne na inaonesha taswira ya maisha ya kila siku ya watu wa matabaka mbalimbali nchini Misri. Pamoja na hayo kuna mtazamo wa mvutano wanaojitahidi kupambana na maisha wakiwa kwenye taifa lao na wale wanaoamini kuwa maisha bora yanapatikana tu nje ya nchi yao. Mazin Yasser, alikuwa miongoni walioipangilia tamthilia hiyo.
‘’Kwangu mimi naona mfululizo huo wa kiswahili mbali na kuwa wa kwanza pia ni kazi ya kipekee kwangu hasa kuhusu mambo ya uelekezaji na kuainisha sehemu mbalimbali za waigizaji wote’’, anasema Mazin.
Baadhi ya mambo yanayojitokeza kwenye tamthilia hii ni ubunifu wake na namna matumizi ya lugha ya Kiswahili yalivyokuwa kwa ufasaha. Imekuwa fursa nzuri kwa wanafunzi ambao wamejifunza lugha ya Kiswahili na kuwa na jukwaa la kuitumia na kuonesha uwezo wao.
Kinachojitokeza ni namna gani vijana waliojitolea na wanavyoonesha matumaini ya kufanya mabadiliko kwa maisha yao wakiwa ndani ya taifa lao. Hamasisho hapa ikiwa kutokuwa na imani ya kwamba mafanikio yanapatikana tu nje ya nchi.
Washiriki kwenye tamthilia hii wanasema imekuwa muamko mzuri kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ain Shams.
‘’Ningetaka kulinganisha kazi yangu hiyo na nyingine lakini kwa kweli sisi ni wa kwanza katika hili’’, alisisitiza Mazin Yasser.
Wanafunzi hao ni wapenzi wa lugha ya Kiswahili, na pia wameamua kuchukua hatua kukabiliana na fikra zinazowatatiza vijana wengi. Pamoja na hayo kubaini kuwa unaweza kuwa na suluhu ya jambo lolote ukiwa katika mazingira ya nyumbani wala siyo kupata fikra ukiwa nje.
Mhadhiri Shaimaa Tarek alieleza kuwa kazi hii ni mwanzo tu wa mfululizo wa kazi za ubunifu zinazowakilisha sauti ya vijana, na kuonesha jinsi lugha na sanaa zinavyoweza kuwa nyenzo za kujieleza, kuhamasisha na kuleta mabadiliko.