Siku ya Jumanne wadau wa soka duniani wameungana baada ya ajali ya gari iliyogonga watu waliokuwa wakisherehekea ushindi wa Liverpool kushinda Ligi Kuu ya England, na kusababisha watu 27 kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Polisi wanasema hakuna uhusiano wowote na ugaidi kufuatia tukio hilo katika mji huo siku ya Jumatatu wakati maelfu walipojitokeza kusherehekea ushindi wa Liverpool licha ya kuwepo kwa mvua kubwa.
Watoto wanne ni miongoni mwa wale waliojeruhiwa, mmoja akiwa amepata majeraha mabaya zaidi, baada ya gari moja kupoteza muelekeo na kugonga watu muda mfupi tu baada ya basi la wazi la wachezaji kupita.
Polisi wamemkamata mwanamume mzungu mwenye umri wa miaka 53.
‘Mkosi’
"Mkosi wakati wa sherehe", liliandika gazeti moja la Uingereza katika ukurasa wake wa mbele siku ya Jumanne, huku gazeti la Daily Mail likiitaja kama "ukatili".
Gazeti la i lilieleza kuhusu "tukio la kushtusha" huku The Guardian likisema kuwa sherehe za klabu hiyo zimekumbwa "na tafrani" kutokana na ajali ya gari hilo.
Gazeti la The Sun limeitaja kuwa "mkosi" huku wadau wa soka duniani wakiungana na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya England.
"Tunawaombea wote waliopatwa na mkasa huu kutokana na tukio hili," Liverpool iliandika kwenye mtandao wa X, ambapo timu kadhaa za Ligi Kuu ziliungana nao katika kuwafariji.
Mahasimu wao Manchester United waliandika: "Tunaungana na LFC na mji wa Liverpool baada ya tukio hilo baya."
Kutoka kwa timu nyingine ya mji wa Liverpool, Everton ilisema: "Tunaungana na wote wale waliotatizwa na tukio hili katika mji wetu."
Mabingwa wa Ligi Kuu ya England walioondolewa katika nafasi yao Manchester City wameandika: "Sote hapa Manchester City tunaungana na wale waliopatwa na ajali hii wakati wa sherehe za ushindi za Liverpool mapema leo."
Nahodha wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard aliweka picha kwenye mtandao wa instagram ya mji huo ikiwa pamoja na kopa jekundu.
‘Kuwafariji na maombi’
Mchezaji wa zamani wa safu ya ulinzi wa Liverpool Jamie Carragher ameandika kwenye mtandao wa X: "Siku imeisha vibaya... naomba iwe kila mtu yuko salama."
Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Gianni Infantino alisema "tunawafariji na kuwaombea wote wale waliotatizwa na ajali hii".
"Wadau wa soka wanaungana pamoja na Liverpool FC na mashabiki wote kufuatia tukio hilo baya wakati wa sherehe za ushindi mjini," alisema katika taarifa.
Picha kwenye mtandao wa kijamii zinaonesha gari hilo likiwa limesimama na kuvamiwa na mashabiki waliokuwa wana hasira, ambao walivunja kioo cha nyuma cha gari wakati polisi wakijaribu kukabiliana nao.
Watu wanne, ikiwemo mtoto mmoja, walikwama chini ya gari.
Chama cha Ligi Kuu ya England kimeandika kwenye mtandao wa X kuwa "kimeshangazwa na tukio hilo la kushtusha".
"Tunawafariji wale wote waliojeruhiwa na kupatwa na msiba huu," walisema.
"Tumekuwa tukiwasiliana na Liverpool FC na tumewafahamisha kuwa tunafuatilia kwa karibu tukio hili."