Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi amesema kuwa mkataba wa amani kati ya nchi yake na Rwanda, unafungua ukurasa mpaya wa utulivu katika eneo la Mashariki mwa DRC.
Taifa hilo, ambalo linasifika kwa utajiri wa maliasili ikiwemo madini, imekumbwa na mapigano ya muda mrefu, yaliyodumu kwa miongo mitatu sasa.
Ijumaa iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na DRC walitiliana saini mkataba wa amani jijini Washington, kama hatua muhimu ya kupata amani ya kudumu Mashariki mwa DRC.
"Mkataba huu unafungua ukurasa mpya wa utulivu na ustawi wa nchi yetu," alisema Rais wa DRC Felix Tshisekedi wakati wa risala yake ya kuadhimisha miaka 65 ya Uhuru wa DRC, siku ya Jumatatu.
Kulingana na kiongozi huyo, mkataba huo ni wa kihistoria na unakuja wakati muhimu wa kumaliza mgogoro katika eneo la Mashariki mwa DRC.
"Huo sio mkataba tu, ni ahadi ya amani kwa watu wetu walioathirika na vita,” alisema Tshisekedi.