Rais wa Kenya William Ruto ameidhinisha Muswada wa Fedha wa 2025 kwa kuutia saini.
Muswada huo ulipitishwa na bunge.
“Muswada huu unatoa fedha za kutosha kusaidia miradi muhimu ya maendeleo nchini katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai 1. Pia utaimarisha utoaji wa huduma kwa kuzingatia vipaumbele vya serikali,” Ikulu ya Kenya imesema.
Muswada wa Fedha 2025 unakuja mwaka mmoja baada ya Muswada wa Fedha 2024 kutupiliwa mbali na Rais Ruto kufuatia maandamano Juni 2024 yaliyoupinga.
Sekta ya afya
Katika Sheria ya Matumizi, sekta ya afya imetengewa zaidi ya dola bilioni moja (shilingi bilioni 133.4 ).
Mfuko wa Kimataifa wa kupambana na maradhi ya ukimwi, malaria na kifua kikuu utapokea dola milioni 133 ( shilingi bilioni 17.3) huku Hazina ya Afya ya Msingi ikitengewa zaidi ya dola milioni 101 ( shilingi 13.1 bilioni).
Zaidi ya hayo, Hazina ya Dharura, Magonjwa Sugu na Muhimu imetengewa zaidi ya dola milioni 61 ( shilingi bilioni), na Mpango wa Chanjo zaidi ya dola milioni 35 (shilingi 4.6 bilioni).
Zaidi ya dola milioni 30 ( shilingi bilioni 4) zitashughulikia mpango wa mafunzo kwa madaktari, zaidi ya dola milioni 39 ( shilingi bilioni 3.8) kwa huduma za afya ya mama na mtoto, huku dola zaidi ya milioni 10 ( shilingi bilioni 1.3 bilioni ) kwa vituo vya saratani na ( zaidi ya dola milioni 13 ( shilingi bilioni1.75 ) za nyongeza ya mishahara ya madaktari kama ilivyoainishwa katika Makubaliano ya Pamoja ya Majadiliano.
Fedha za kilimo
Ili kuongeza tija, kusaidia wakulima na kuifanya Kenya kuwa na uchumi unaojikita katika kupata chakula cha zaidi, dola zaidi ya milioni 360 ( shilingi bilioni 47.6) zimetengewa kilimo.
Zaidi ya dola milioni 78 ( shilingi milioni 10.2) zimetengwa kwa ajili ya Mradi wa Kitaifa wa Kukuza Thamani ya Kilimo ili kubadilisha wakulima wadogo katika kaunti 33 kutoka kilimo cha kujikimu hadi cha kibiashara kupitia ongezeko la thamani na upatikanaji wa soko.
Takriban dola milioni 60 (shilingi bilioni 8) zimetengwa kwa ajili ya Mpango wa Ruzuku kwa mbolea ili kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo nafuu na bora kwa wakati unaofaa.
Wakati huo huo, zaidi ya dola milioni 30 (shilingi bilioni 4 bilioni) zimetengewa Mfuko wa Kuondoa Deni la Kahawa na Hazina ya mbegu ili kusaidia kukuza kilimo cha kahawa kote nchini.
Biashara
Kwa kutambua changamoto zinazokabili makampuni madogo katika kupata mikopo ya bei nafuu, Muswada huu unatoa zaidi ya dola milioni 10 (shilingi bilioni 1.3) kwa Mpango wa Ujumuishaji wa Kifedha wa Vijijini Kenya na zaidi ya dola milioni mbili (shilingi milioni 300) kwa mfuko wa kutoa mikopo midogo midogo maarufu ‘Hustler Fund’.
Mgao huo utaongeza ukuaji wa biashara na kuongeza upatikanaji wa ufadhili kwa watu wa kipato cha chini.
Katika hatua inayolenga kujenga uhusiano kati ya mabadiliko ya kilimo, maendeleo ya biashara ndogo ndogo na uzalishaji, sheria inatoa zaidi ya dola milioni 139 (shilingi bilioni 18) kupitia mashirika mbalimbali.
Vipengele muhimu ni pamoja na zaidi ya dola milioni 37 (shilingi bilioni 4.5) kwa ajili ya kuanzishwa kwa Hifadhi za Kaunti ya Viwanda vya kuimarisha bidhaa za kilimo na zaidi ya dola milioni 8.5 (shilingi bilioni 1.1) kwa ajili ya kuendeleza kongano la viwanda vya nguo katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi huko Naivasha na Athi River.
Wakati wa hafla hiyo katika Ikulu ya Nairobi, Alhamisi Naibu Rais Kithure Kindiki, viongozi waandamizi wa Bunge wakiongozwa na Spika Moses Wetang’ula, Waziri wa Fedha John Mbadi, miongoni mwa wengine, walihudhuria.