Ikipambwa kwa ngoma za tamaduni na historia mbalimbali, Mei 25 ya kila mwaka, ni siku ya kipekee barani Afrika.
Ni siku ambayo, jamii zote za Waafrika, ndani ya bara lenyewe na waliopo ughaibuni, hukusanyika pamoja, kuadhimisha ‘Siku ya Afrika’.
Miaka 67 iliyopita, baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika ambazo zilikuwa zimejipatia uhuru, walikusanyika nchini Ghana kwa ajili ya mkutano wao.
Ulikuwa ni mkutano wa kipekee ulioangazia ustawi wa bara lililo huru.
Wakati wa mkutano huo, wajumbe walipendekeza iwepo ‘Siku ya Uhuru wa Afrika’, kuenzi vuguvugu la ukombozi na kuimarisha mshikamano kwa nchi ambazo zilikuwa hazijakombolewa kutoka kwenye minyororo ya ukoloni.
Vuguvugu hilo lilizidi kuongezeka kadiri nchi za Afrika zilivyozidi kupata uhuru, kabla ya maamuzi makubwa kufikiwa Mei 25, 1963.
Jumla ya mataifa 32 huru barani Afrika yalikutana jijini Addis Ababa, Ethiopia, na kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo Kwame Nkrumah, Julius Nyerere, Haile Selassie, Gamal Abdel Nasser, Abubakar Tafawa Balewa, Sékou Touré, Leopold Senghor, na kuja wazo hilo.
Kulingana na Umoja wa Afrika, siku hii haitumiki kwa tafakuri tu, bali kujenga mustakabali wa Afrika.
Siku hii hukumbushia namna wapigania uhuru walivyojitolea maisha yao kwa ajili ya ukombozi wa bara lao.
Miaka mingi baadae, bara la Afrika limetengeneza ajenda yake ya mwaka 2063.
Hasara za Ukoloni
“Tunapoadhimisha siku hii, tunakumbuka uafrika wetu, mila, desturi, nguvu na umoja wetu, tukinuia kupata haki na fidia kwa ustawi wa waafrika wote popote walipo,” anasema Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf.
Kauli mbiu ya mwaka huu inaangazia haki na fidia.
‘‘Kauli mbiu ya mwaka huu inadhihirisha kiu ya bara la Afrika ya kufunga ukurasa wa mateso iliyopitia wakati ule na inayoendelea kupitia kwa sasa, na kujenga kesho yenye utu na usawa,” mtaalamu wa mambo ya diplomasia Abdoul Fathi Sanogo, anaiambia TRT Afrika.
Nchini Uturuki, Asasi Isiyo ya Kiserikali ya ‘Umoja wa Marafiki wa Afrika’(TADD) na Chuo Kikuu cha Istanbul, kiliandaa tukio la kuadhimisha ushirikiano kati ya Uturuki na nchi za Afrika, lililofanyika jijini Istanbul.
Tukio hilo liliwakutanisha pamoja wanajopo mbalimbali ambao walijadili masuala ya uhusiano na maendeleo ya bara la Afrika.
"Tunazungumzia historia ya Afrika, ukoloni mambo leo na masuala mbalimbali. Leo niliamua kuzungumzia teknolojia kama chachu ya maendeleo ya Afrika," anasema Mustapha Aminu Tukur, msomi anayesomea udaktari wa falsafa kutoka chuo cha Yildiz, katika mahojiano yake na TRT Afrika.
"Ina maana sana kuwepo hapa kwani ni fursa ya kujadili masuala ya Waafrika waliopo Uturuki na kwingineko," anasema Faroukou Mintoiba, mkuu wa Bizim Afrika, shirika lililopo nchini Uturuki.
Kukua kwa uhusiano na Uturuki
Nchi nyingi barani Afrika zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile mzigo wa madeni na zinginezo.
Kutokana na ukweli, nchi nyingi kwa sasa zinaangalia fursa zingine, mbali na nchi za magharibi, kama vile Uturuki na Urusi.
Kwa mfano, ushirikiano kati ya Uturuki na Afrika, umezidi kukua na kuimarika, toka Uturuki ilipoutangaza mwaka 2005, kuwa “Mwaka wa Afrika."
Nchi hiyo imeongeza mahusiano yake ya kidiplomasia, ikizidi kufungua balozi zake barani Afrika, huku ikipata hadhi ya uangalizi ndani ya Umoja wa Afrika, mwaka 2008.
Moja ya maeneo ambayo Uturuki imewekeza nguvu ni kukuza uhusiano wake na nchi za Afrika hasa katika nyanja ya elimu, ambapo maelfu ya wanafunzi kutoka Afrika wanasema nchini Uturuki kwa ufadhili.
“Wanafunzi hawa ni moja ya nguzo muhimu ya kujenga Afrika iliyo imara na kukuza uhusiano na Uturuki, anasema Bilgehan Güntekin, Rais wa Umoja wa Marafiki wa Afrika.