Kocha wa klabu ya Manchester City ya England, Pep Guardiola, amemsifu kocha wa Al Hilal ya Saudi Arabia, Simone Inzaghi, baada ya timu yake kuwachakaza vijana wa Cityzens kwa mabao 4-3 katika muda wa nyongeza na kuiondoa kwenye Kombe la Dunia la Vilabu.
Mhispania huyo alikiri kuwa timu ya Inzaghi iliwazidi mbinu kupitia mashambulizi ya kushtukiza.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 2-2 katika muda wa kawaida siku ya Jumatatu, lakini katika dakika za mwisho za muda wa nyongeza uliojaa matukio, Marcos Leonardo alifunga bao la ushindi na kuiwezesha Al Hilal kupata mojawapo ya ushindi muhimu zaidi katika historia ya soka Mashariki ya Kati.
Kwa ushindi huo, Al Hilal imefuzu hatua ya robo fainali ambapo itakutana na klabu ya Fluminense ya Brazil, ambayo iliwafunga Inter Milan 2-0 na kufufua matumaini ya timu isiyotoka bara Ulaya kufika hatua ya nusu fainali.
“Tulijua kwamba tunahitaji kufanya jambo lisilo la kawaida ili kuishinda Manchester City na ndivyo vijana wangu walivyofanya. Walikuwa na mchezo mzuri sana,” alisema Inzaghi baada ya ushindi huo wa kushangaza huko Orlando.