ULIMWENGU
6 dk kusoma
Kusitishwa kwa misaada ni janga la kimaadili na kimkakati kwa watoto duniani
Kusitishwa kwa misaada kutoka nje kumesababisha kuchukuliwa kwa maamuzi magumu, kuongeza mgogoro duniani, na kufanya maisha ya mamilioni ya watoto kuwa hatarini—yote haya yakiwa ni ukosefu wa maadili na kukosa dira ya kimkakati.
Kusitishwa kwa misaada ni janga la kimaadili na kimkakati kwa watoto duniani
Watoto, kama wa wakimbizi wa Rohingya wakila kutoka kwenye madumu ya nembo ya USAID katika kambi moja mjini Cox's Bazar, Bangladesh, 11 Februari, 2025, wataathirika zaidi na kusitishwa kwa misaada (Reuters/Ro Yassin Abdumonab). / TRT World
19 Machi 2025

Na Gabriella Waaijman

Nikiwa kama mtu anayeshughulika na masuala ya misaada, ninafahamu kuwa kazi yangu inasaidia kubadilisha maisha ya mamilioni ya watoto. Ni msingi kuwa maisha ya watu wote yana thamani sawa ambayo yananipa mimi ari pamoja na wafanyakazi wenzangu wa mashirika ya misaada, hata wakati tunakabiliwa na changamoto.

Na leo hii, tunakabiliwa na tatizo kubwa kuliko tulivyotarajia: kuwa kwenye njia panda ya kuamua maisha gani ya kuokoa na gani ya kuyaacha.

Kusitishwa kwa misaada kutoka nje hivi karibuni kumesababisha mashirika ya misaada kufanya maamuzi magumu. Katika kipindi ambacho mtoto mmoja kati ya 11 kote duniani anahitaji msaada, tunalazimishwa kuamua tatizo gani ni kubwa kuliko lingine, jamii moja kuliko nyingine, na hadi maisha ya mtoto mmoja kuliko ya mwingine.

Tayari, imebidi tufanye maamuzi magumu kusitisha miradi ya kuokoa maisha ya watu. Kwa hili, tiba kwa watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo au usaidizi muhimu kwa watoto wanaozaliwa katika mazingira ya vita. Hili siyo tu suala la kuwafikia waliko’, ni suala la kimaadili zaidi ambalo linatugusa kabisa katika kazi zetu, na kwa yote yale ambayo tunaamini.

Hatari kwa misingi


Shirika la Save The Children lilianzishwa zaidi ya karne moja iliyopita na Eglantyne Jebb, mwanamke mmoja jasiri. Alianzisha shirika ambalo litashughulikia kutetea haki za watoto, kuokoa maisha, kulinda familia, ili kuwaondolea madhila, na kuhakikisha heshima yao inadumu.

Leo hii, tuko katika mataifa 115, tukisaidia moja kwa moja zaidi ya watoto milioni 105 kila mwaka. Mara nyingi tunakuwa wa kwanza katika kusaidia panapokuwa na dharura, na dhamira yetu kwa kila mtoto, kila mahali, haiwezi kupingika.

Katika wakati ambao mizozo inaongezeka duniani — mapigano, mabadiliko ya hali ya hewa, na hali mbaya ya uchumi — mataifa mengi tajiri duniani yanapunguza bajeti zao za misaada. Marekani, Uingereza, Ujerumani, Australia, Sweden, Denmark, Ufaransa, Uholanzi na nchi zingine ambazo kawaida huchangia pia zinajiondowa katika ahadi zao za kuungana na jumuiya ya kimataifa, jambo linalosababisha kupungua kwa sehemu kubwa ya misaada kote duniani.

Kusitisha misaada siyo tu suala la kimaadili katika uongozi, ila ni kosa la kimkakati.

Kushindwa kukabiliana na umaskini, ukosefu wa usalama, na matatizo ya afya kote duniani kunasababisha kuongezeka kwa matatizo kote ulimwenguni, kufanya watu kuhama makazi yao, kudorora kwa uchumi, na migogoro. Matatizo haya huwa hayazingatii mipaka; yanaathiri kila mahali. Na tunapowasahau wale walio kwenye hatari zaidi, tunajenga misingi ya matatizo ya baadaye ambayo hatimae yatafika katika maeneo yetu, na siku zote watoto ndiyo wanaoumia zaidi.


Mwaka 2024, watu milioni 120 walilazimika kuhama makazi yao kutokana na vita, ghasia na mateso - takriban sawa na idadi ya watu nchini Japan - na watu waliondolewa kwenye makazi yao wakiwa nje ya maeneo kwa wastani kwa kipindi cha muongo mmoja. Mara nyingi, wanatuambia lengo lao ni kurejea kwao. Misaada huwa na nafasi kubwa katika kuwasaidia watu kurejea makwao.

Nchini Ukraine, tumesaidia familia kama za kina Natalia* na binti yake Sofiya* kukarabati nyumba yao iliyokuwa imeharibiwa. Huko Ethiopia, tumewasaidia wanawake kama kina Rukia* kuanzisha biashara ndogo ndogo na kurejea tena katika hali ya kawaida. Misaada inasaidia kujenga jamii, kuimarisha usalama, na kusaidia katika kuimarisha hali ya uchumi. 

Misaada inawasaidia watu waliokwama kutokana na kuondolewa katika makazi yao, ambao hawana pa kwenda. Kama Aliya* na Zahra*, wasichana wawili walioko katika kituo cha Al Hol nchini Syria. Wamelelewa hapo. Hawakubaliki katika nchi zao, nyuso zao zinaonesha ishara ya matumaini, na macho yao yakidhihirisha hali tofauti ya jukumu la jambo ambalo wao hawakuhusika.

Kutofikiria kwa makini

Maamuzi ambayo hayajafikiriwa kwa makini ya kusitisha misaada yanafanya dunia kutokuwa na watu wenye afya, kutokuwa salama, na kukosa maendeleo. Idadi ya watoto wanaoishi katika maeneo ya vita imeongezeka maradufu katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 iliyopita, ilhali matumizi ya kijeshi duniani kote yameongezeka hadi dola trilioni $2.4 mwaka 2023. Wakati huohuo, uwekezaji katika suala la kuzuia mapigano na kusaidia watu unapungua.

Mwaka 2025 kumekuwa na wito wa kupatikana kwa dola bilioni $44.7 kwa ajili ya kusaidia watu 190 katika mataifa 32 na kanda tisa zilizo na wakimbizi. Kama fedha hizi zote zitapatikana, itakuwa kiasi cha dola $235 kwa mtu mmoja kila mwaka, dola $20 kwa mwezi, au senti 65 za Marekani kwa siku, hiyo ni chini ya bei ya kikombe kimoja cha kahawa katika mataifa mingi ya Magharibi. 

Wito wa mchango wa 2024 ulifanikiwa kwa asilimia 45. Kusema misaada haina ufanisi siyo sahihi na pia ni njia moja ya kupindisha mitazamo ya watu .  

Gaza, Haiti, na Sudan, maafisa wetu wanakabiliwa na idadi ya watoto —wengine ambao hata hawajaanza kwenda shule —wanaohitaji msaada wa kisaikolojia kutokana na kushuhudia ukatili ambao haufai kwa mtoto yoyote kupitia hayo.

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, makundi yenye silaha yanawalenga watoto na kuwateka ili wajiunge katika mapigano. Hatuwezi kusema hatuoni hili tatizo.

Uwekezaji katika suala la maendeleo na misaada kwa watu siyo tu jambo la kusaidia—ni mkakati muhimu na zaidi jukumu la kimaadili. Kusitisha misaada kutaongeza matatizo, na kusababisha ukosefu wa usalama ambapo itagharimu zaidi katika kukabiliana na hali hiyo baadaye.

Maamuzi magumu


Huku misaada ikisitishwa, wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanalazimika kufanya maamuzi magumu: Tuwape chakula watoto katika maeneo ya njaa kali au tuwapelekee matibabu wale walio katika maeneo ya vita? Tuangazie kuokoa watu kwenye mafuriko au tuwekeze katika masuala ya tabianchi? Kila maamuzi yanamaanisha baadhi ya watu watapata misaada ya kuokoa maisha yao — na wengine hawatopata huduma hizo. 

Mzigo huu unawalemea sana wafanyakazi wote wa mashirika ya misaada. Shirika la Save the Children linaamini kuwa kila mtoto ana haki sawa, lakini ukweli ni kuwa wakati misaada ikisitishwa, watu wanapoteza maisha.

Mambo kote duniani yanabadilika, mataifa mengine yenye uwezo, miungano mbalimbali, na kuongezeka kwa hali ya wasiwasi. Mabadiliko haya yanaleta matatizo zaidi kwa kazi zetu. Suala hapa siyo kama tunaweza kuendelea kutoa misaada - ni kuhusu kama tutaweza kuishi bila misaada. Hiki ni kipindi ambacho kinahitaji watu kuja pamoja na kushirikiana. Bila ya hivyo, kuna hatari ya kurejesha nyuma hatua zote zilizopigwa kwa miongo kadhaa katika kudhibiti umaskini, afya, na elimu.

Serikali zina jukumu muhimu la kuendeleza juhudi za kutoa misaada. Hatuwezi kuendelea na mtindo huu ambapo kuokoa maisha mengine kunamaanisha kupoteza maisha ya baadhi ya watu. Kwa sababu ni vigezo gani vinatumika kuamua maisha ya mtu hayana thamani?

Ni wakati wa kutafakari tena kuhusu dunia ambayo imejaa huruma na jumuiya ya kimataifa kuhamasisha ushirikiano kati ya jamii—dunia ambayo maisha ya kila mtoto yanaheshimika.

*Majina yamebadilishwa ili kuwalinda watoto hao.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us