ULIMWENGU
6 dk kusoma
Mashambulizi ya Israeli yanayoongezeka Gaza ishara ya hali mbaya kwa watu
Israeli imeendeleza mashambulizi yanayolenga kuwadhoofisha kisiasa, na kuacha Gaza ikikabiliana na hali mbaya kwa watu.
Mashambulizi ya Israeli yanayoongezeka Gaza ishara ya  hali mbaya kwa watu
Mamia ya Wapalestina wameuawa katika mashambulio ya Israeli yanayoendelea huko Gaza (Husam Maarouf). / others
26 Machi 2025

Gaza - Mashambulizi yaliyoanza tena Gaza hayakuanza tu hivi hivi. Ni mkakati wa kijeshi uliopangwa mahsusi na ambao una ujumbe wa kisiasa, na hali mbaya kwa watu ambayo inazidi kuwa hatari. 

Ndani ya saa 24, Wapalestina zaidi ya 400 wameuawa katika moja ya mashambulizi mabaya kutokea kipindi cha miezi 16 ya vita, ikionesha mabadiliko makubwa ya msimamo wa Israeli katika majadiliano na mbinu za kivita.

Kuongezeka kwa ghafla mashambulizi haya ya kijeshi ni kutokana na kauli ya afisa mmoja mwandamizi wa Hamas Osama Hamdan alipowashtumu Israeli kwa kubadilisha misimamo kuhusu makubaliano.

Kulingana na Hamdan, mapendekezo yaliyokuwepo awali yaliyoongozwa na Mmarekani Adam Boehler yalibadilishwa na mjumbe wa Marekani Steven Witkoff.

Mapendekezo mapya, Hamdan anasema, yanakiuka misingi ya awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano na yanaondoa vipengele muhimu ikiwemo wanajeshi wote wa Israeli kuondoka Gaza, pamoja na kuondoa vifusi ili kusaidia katika juhudi za ujenzi upya wa eneo hilo.

Kuanzisha tena mashambulizi kwa Israeli kunaonesha majadiliano sasa yataendeshwa kwa mtutu wa bunduki na wala siyo kwa njia ya mashauriano.

Mauaji yanayolenga watu mahsusi kama silaha ya kisiasa

Mashambulizi ya hivi karibuni yalilenga kudhoofisha uwezo wa uongozi wa kundi la Hamas kisiasa na kijeshi.

Miongoni mwa wale waliouawa ni Yasser Harb, mwanachama wa idara ya siasa ya Hamas; Abu Ubaida al-Jamasi, kiongozi mwingine mwandamizi wa Hamas; Abu Hamza, msemaji wa kikosi cha Al-Quds; na Mahmoud Abu Watfa, afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya ndani inayosimamiwa na Hamas. 

Mashambulizi haya yameleta kumbukumbu ya mkakati wa Israeli wa kuwaua viongozi wa Hezbollah, wakilenga kusambaratisha mifumo yao ya uongozi na kuidhoofisha.

Lengo lao liko wazi: kuleta hofu, huku wakidhoofisha uwezo wa uongozi wa Hamas na kuweka shinikizo kwa kundi hilo liweze kukubali mapendekezo yao — hasa katika kuwaachilia huru mateka bila kuachiwa wafungwa Wapalestina walioko katika jela za Israeli — jambo ambalo Hamas haiwezi kukubali.

Majadiliano kwa kuweka shinikizo

Mashambulizi haya yaliyoongezeka ni mbinu ya kubadilisha muelekeo wa majadiliano kwa kutumia nguvu ya kijeshi.

Mkakati huu unaangazia mfumo mpana wa diplomasia ya Israeli: ukitaka kupeleka muelekeo kwa njia ya vita wala siyo kwa makubaliano ya pande zote.

Njia hii inafanya hali kuwa ngumu zaidi, kuifanya Hamas iendelee kujitetea na pengine kuharibu uwezekano wa kupatikana kwa makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano.

Wakati huo huo, hali kwa watu inazidi kuwa mbaya —mauaji ya raia wengi, watu kuondolewa katika makazi yao ya
Beit Hanoun na Khan Younis, na uharibifu wa miundombinu muhimu — kunaendelea kuwapa shinikizo Hamas, kwa lengo la kuwafanya wakubali matakwa yao.

Lakini historia inaonesha kuwa mfumo huu unachochea watu kujilinda zaidi na kuzidisha machafuko.

Athari za kitaifa na kimataifa

Marekani pia inahusika katika mashambulizi haya. Taarifa zilizothibitishwa za Ikulu ya Marekani zinaonesha kuwa kulikuwa na majadiliano kabla, ishara kuwa mikakati ya mashambulizi ya Israeli dhidi ya Hezbollah yalipata msaada wa Marekani.

Lengo la kisiasa linaendana na nia za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Rais Donald Trump walivyoeleza kuwa wanataka kuvunja mfumo wa kisiasa wa Hamas na kuwepo Gaza baada ya vita vya eneo hilo.

Katika mazungumzo ya siri, majadiliano kuhusu mustakabali wa utawala wa Gaza, mipango ya uwekezaji wa eneo hilo, na hata kuwatimua watu kutoka katika makazi yao yanaendelea —ishara kuwa hivi si vita tu, bali maandalizi ya kubadilisha mfumo mzima wa sehemu hiyo.

Kuzidi huku kwa mashambulizi pia kuna athari kubwa kwa siasa za ndani ya Israeli, hasa kwa kuruhusu kurejea kwa mwanasiasa wa mrengo wa kulia Itamar Ben-Gvir kama Waziri wa Mambo ya ndani - hatua ambayo Waziri Mkuu Netanyahu anaiona kama ni muhimu kimkakati.

Ben-Gvir, anayejulikana kwa misimamo yake mikali, anaunga mkono sera kandamizi za usalama, kupanua maeneo ya ulowezi, na hatua kali zaidi dhidi ya watu wa Palestina.

Kurejeshwa kwake siyo tu ishara ya kawaida ila ni mkakati wa kumuwezesha Netanyahu kupata kuungwa mkono kisiasa kwa ajili ya kupitisha bajeti ya taifa ya Israeli kufikia 31 Machi, 2025.

Kwa hiyo mpango huu wa Netanyahu una malengo mawili: Uwezo wa kijeshi nje ya taifa lake na kuendelea kubaki madarakani.

Kurejea kwa Ben-Gvir kwa nafasi hiyo huenda ikawa ishara mbaya kwa Wapalestina, ambapo kunatarajiwa kuongezeka kwa shughuli za walowezi, kuzidi kwa mashambulizi, na kumaliza zaidi haki za kimsingi na za kisiasa za Wapalestina.

Matatizo kwa watu

Wakati wanapanga njama za kisiasa na mikakati ya kijeshi, hali inazidi kuwa mbaya kwa watu wa Gaza.

Kufikia 2, Machi 2025, hakuna chakula kilichokuwa kimeingia Gaza, kuongeza hofu ya baa la njaa. Ramadhan, ambayo kawaida ni kipindi cha kupata mazingatio kiimani , imebadilika na kuwa ya njaa na huzuni.

Hakuna bidhaa sokoni, na zile chache zilizobaki bei yake imekuwa mara tatu zaidi. Hakuna fursa za ajira tangu vita vilipoanza, na watu hawana njia za kuwaingizia mapato.

Walionusurika wanaishia kwenye mahema ya muda, kando ya mitaro ya maji machafu na kuhofia mashambulizi ya mara kwa mara. Israeli imekuwa ikizuia juhudi za ujenzi upya, na hivyo kusababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Huku ikiwa hakuna maji safi kwa kipindi cha zaidi ya miezi 18, mfumo wa afya wa Gaza unaelekea kuporomoka, na hofu ya vifo vingi kutokana na njaa na maradhi.

Upatanishi

Katika juhudi za kukabiliana na hali hii, Misri ilialika ujumbe wa Hamas mjini Cairo, wakijaribu kusaidia katika majadiliano ya kusitisha mapigano na kuepusha vita zaidi.

Hata hivyo, kwa kutizama mashambulizi ya sasa ya Israeli na malengo yake, uwezekano wa kusitisha mapigano ni mdogo.

Bado, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini mashambulizi yakiendelea mfululizo kwa wiki nzima, kutalazimika kuwa na hatua nyingine ya mazungumzo. Pande zote mbili zinataka kuafikiana kuhusu kubadilishana mateka na wafungwa.

Yanayofanyika kwa sasa Gaza yanadhihirisha mabadiliko makubwa ya namna vita vinavyopiganwa na diplomasia. Israeli inaonekana kutumia mashambulizi zaidi siyo tu kama silaha ya kijeshi, bali pia ni njia ya mawasiliano kuhusu majadiliano.

Kupitia mashambulizi, mauaji ya watu mahsusi, na kuwakandamiza watu, ni kujaribu kubadilisha muelekeo kwamba uwezo wao si kupitia mazungumzo ila ni kupitia uharibifu.

Kile kinachosubiriwa ni kama mkakati huu utasaidia upatikanaji wa suluhu ya kudumu au utazidisha msururu wa machafuko, makabiliano, na dhiki.

Kwa vyovyote vile, ujumbe uko wazi: Katika Gaza ya leo, diplomasia inafanyika kupitia mtutu wa bunduki, na wanaouawa zaidi ni raia wa kawaida.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us