Swansea City imetangaza kuwa mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or Luka Modrić amejiunga na klabu hiyo kama muwekezaji na mmoja wa wamiliki.
Timu hiyo ya Wales yenye makao yake katika mji wa Swansea, Uingereza, ilimuelezea Modrić kama mfano mzuri wa kuigwa.
“Nina furaha kwa kuwa Luka amejiunga na sisi kama muwekezaji na mmiliki mwenza. Hakuna mtu ambaye ni mfano mzuri kwa wachezaji wetu kwenye mchezo huu kama Luka, kuanzia katika vituo vyetu vya mafunzo mpaka kwenye timu A," alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa Swansea Tom Gorringe siku ya Jumanne.
Modrić, raia wa Croatia, ni nahodha wa timu ya La Liga ya Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia.
Mchezaji aliyepata mataji mengi zaidi
Ni mchezaji aliyeshinda mataji mengi zaidi katika historia ya Real Madrid, akiwa ameshinda nao ligi ya mabingwa barani Ulaya mara sita, mataji sita ya dunia kwa mashindano ya vilabu, makombe matano ya Super Cup Ulaya, na Ligi kuu ya Uhispania mara nne, makombe mawili ya Uhispania, na mara tano akanyayua makombe ya Super Cup ya Uhispania.
Mchezaji huyo kiungo mwenye umri wa miaka 39 ametaja kujihusisha kwake na Swansea kama “fursa nzuri sana”.
“Swansea inatambulika sana, ina mashabiki wengi, na ari ya kucheza katika hatua ya juu ya ligi. Kucheza kwenye kiwango cha juu cha ligi, naamini naweza kuchangia uzoefu wangu kwa klabu,” Modrić alisema katika taarifa.
Bodi ya Swansea ilisema kwa pamoja, “Tumefurahi kuwa Luka amejiunga na sisi wamiliki. Kutoka kwa mazungumzo yetu ya kwanza, ilikuwa wazi kuwa tulikuwa na mtazamo sawa wa dira yetu na kwamba Luka angekuwa mtu sahihi kwa bodi yetu.”
Modric pia ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa FIFA, Ballon d’Or mwaka 2018, na alicheza kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2018.
Ni mchezaji aliyechezea Croatia mara nyingi zaidi, na akiwa na umri wa miaka 39, tayari amecheza mara 45 kwa Real Madrid msimu huu, na kufunga magoli manne.