Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Klabu ya Yanga SC kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (NBC Premier League) msimu wa 2024/2025.
Katika hafla ya kukabidhi zawadi iliyofanyika Jumatatu Ikulu ya Zanzibar, Dkt. Mwinyi aliikabidhi timu ya Yanga zawadi ya shilingi milioni 100 za Tanzania, kama sehemu ya pongezi kwa mafanikio yao makubwa.
Wakati wa hafla hiyo, timu ya Yanga pia ilimkabidhi Rais Mwinyi makombe matano waliyoyatwaa msimu huu kutoka kwenye mashindano mbalimbali.
Dkt. Mwinyi alieleza kuwa mafanikio hayo si tu yanaiinua hadhi ya klabu hiyo, bali pia yanajenga heshima na historia katika tasnia ya michezo nchini.
Aidha, aliishkuru Yanga kwa kuitangaza Zanzibar kupitia kampeni ya 'Visit Zanzibar' pamoja na hatua ya kucheza baadhi ya mechi zao visiwani humo, akisema imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na sekta ya utalii wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said Ali, alimpongeza Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake madhubuti katika kuimarisha miundombinu ya michezo visiwani.
Pia alimkabidhi Rais Mwinyi medali maalum ya kombe la CRDB na jezi ya ubingwa wa Ligi Kuu kama ishara ya kutambua mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini.