Msichana mwenye umri wa miaka kumi na nne aliuawa na simba nje ya hifadhi ya Nairobi, na mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 54 amefariki baada ya kuvamiwa na ndovu, Mamlaka ya Wanyamapori ya Kenya (KWS) ilisema.
Kulingana na KWS, tukio la kwanza, lilitokea katika shamba moja upande wa kusini wa hifadhi ya Nairobi, ambapo msichana wa umri wa miaka 14 aliuawa na simba.
“Kama saa moja usiku hivi, KWS ilipata taarifa kuwa simba ameingia kwenye eneo la makazi ya watu la Savannah, lililoko upande wa pili wa hifadhi hiyo ya Nairobi, na kumshambulia msichana —wa darasa la 7 katika shule moja ya msingi.”
Kijana mwingine alishuhudia shambulizi hilo, ambapo alipiga kamsa kuita watu, maafisa wa Mamlaka ya Wanyamapori wa Kenya walifika eneo hilo kwa ajili ya kutoa msaada.
Simba hatari
Maafisa “walifuatilia alama za damu hadi katika mto Mbagathi, ambapo mwili wa msichana ulipatikana ukiwa na majeraha katika sehemu ya mgongoni”. Simba huyo hakupatikana karibu na eneo hilo.
Mamlaka ya KWS inasema iliweka mtego na kutuma maafisa kumtafuta simba huyo.
“Juhudi zinaendelea katika kuimarisha hatua za usalama na kuepusha matukio mingine kama hayo.”
Kwingineko KWS inasema mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 54 alishambuliwa na ndovu katika kaunti ya Nyeri, ndani ya msitu wa Mere.
Mwanamume alipata majeraha ya kifua, na kuvunjika mbavu “ lakini kwa bahati mbaya alifariki baadaye”.
“Mamlaka ya Wanyamapori ya Kenya inasikitika kuthibitisha kuwa mzozo wa binadamu na wanyama umesababisha vifo vya watu wawili.”
Kuzuia mizozo
Shirika hilo limesisitiza umuhimu wa “kuendelea kuwekeza katika hatua za kuzuia mizozo kati ya binadamu na wanyama — kupitia mikakati muhimu, mifumo ya kutoa onyo mapema, na kuimarisha ushirikiano na jamii zilizoathirika.”
Mashambulizi ya wanyama hayafanyiki mara kwa mara lakini yanapotokea yanasababisha vifo.
Mwezi Februari, fisi walimuua mwanamume mmoja na kuwajeruhi watu wawili karibu na chuo kimoja kikuu viungani mwa makao makuu ya Kenya, kusababisha mamia ya wanafunzi kutoka chuo hiko kuandamana wakilalamikia kuhusu ukosefu wa usalama.