AFRIKA
3 dk kusoma
Wagombea wanne wa upinzani Côte d'Ivoire wazuiliwa kushiriki uchaguzi wa rais Oktoba
Viongozi wanne wa upinzani nchini Côte d'Ivoire wameondolewa kwenye orodha ya mwisho ya wagombea urais mwezi Oktoba 2025.
Wagombea wanne wa upinzani Côte d'Ivoire wazuiliwa kushiriki uchaguzi wa rais Oktoba
Tidjane Thiam, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Cote d’Ivoire, ni miongoni mwa watia nia ya urais waliopigwa marufuku. / Picha: Reuters
4 Juni 2025

Viongozi wanne wa upinzani nchini Côte d'Ivoire majina yao yameondolewa kwenye orodha ya mwisho ya wagombea, maafisa walitangaza siku ya Jumatano, na kuwaacha nje ya uchaguzi wa urais wa baadaye mwaka huu.

Tidjane Thiam, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, Democratic Party of Côte d'Ivoire (PDCI), jina lake liliondolewa kwenye daftari la wapiga kura mwezi Aprili baada ya uamuzi wa mahakama kueleza wasiwasi kuhusu uraia wake wa Côte d'Ivoire wakati alipojisajili.

Rais wa zamani Laurent Gbagbo, na mpambe wake wa karibu Charles Ble Goude na aliyekuwa Waziri Mkuu ambaye yuko uhamishoni Guillaume Soro kwa miaka kadhaa sasa wamepigwa marufuku kushiriki kutokana na kupatikana na hatia na majina yao hayakuwekwa kwenye orodha.

Hakuna hata mmoja wao ambaye ataweza kugombea uchaguzi wa urais wa Oktoba 25 au hata kupiga kura.

Jina la Rais lipo

Rais Alassane Ouattara, 83, ambaye amekuwa madarakani tangu 2011, jina lake lipo katika daftari la wapiga kura lakini bado hajatangaza kama atagombea muhula wa nne au la.

Mwaka 2015 na 2020, Ouattara alishinda kura kwa zaidi 80%.

Mkuu wa tume ya uchaguzi Ibrahime Kuibiert Coulibaly alitangaza Jumatatu kuwa hakuna tena mabadiliko yatakayofanyika kwa daftari la wapiga kura kabla ya uchaguzi.

"Kuondolewa kwangu katika orodha ya wapiga kura na tume ya uchaguzi ni jambo la kusikitisha lakini mfano mzuri wa kuonesha namna Côte d'Ivoire ilivyo mbali na demokrasia," Thiam alisema katika taarifa siku ya Jumatano.

Marufuku kwa upinzani

Mfanyakazi huyo wa zamani wa benki ya kimataifa, ambaye amekuwa nje ya Côte d'Ivoire kwa zaidi ya miezi miwili, ametoa wito kwa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, chama chake kimesema.

Wakili wake Mathias Chichportich amesema katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP kwamba kumnyima kiongozi wa upinzani "haki zake za kisiasa" ilikuwa "ukiukwaji mkubwa wa dhamira ya kimataifa ya Côte d'Ivoire."

Kwa upande wake, chama cha Gbagbo cha African Peoples – Côte d'Ivoire (PPA-CI) – kimelalamika kuwa mamlaka "hazikusikiliza ushauri, wala wito wa kujadiliana", katibu wao mkuu Jean-Gervais Tcheide aliiambia AFP.

"Ni aibu kwamba wamelazimisha orodha hii," alisema, akiongeza: "Hatutowaruhusu wafanye hivyo."

Mke wa rais wa zamani aruhusiwa kugombea

Wagombea wengine wa upinzani ambao wametangaza nia yao ya kugombea urais majina yao yako kwenye orodha ya mwisho ya wapigaji kura.

Wanajumuisha mke wa rais wa zamani Simone Ehivet Gbagbo, ambaye, akizungumza kwa niaba ya muungano wa upinzani, alisema mazingira siyo mazuri ya uchaguzi wa "amani, na utulivu."

Kuibiert Coulibaly, mkuu wa tume ya uchaguzi, ametoa wito wa kuheshimu maamuzi ya mahakama na "kumaliza tofauti zote" na kufanya Côte d'Ivoire "kuwa taifa linaloongozwa kwa utawala wa sheria."

Katika uchaguzi wa urais wa 2020, mabadiliko ya daftari la wapiga kura yalifanyika mwezi Juni kabla ya uchaguzi wa mwezi Oktoba.

Karibu wapiga kura milioni tisa wamejisajili

Kuna jumla wa wapiga kura milioni 8.7, katika nchi ambayo ina wahamiaji wengi na ambapo karibu nusu ya raia wake milioni 30 wako chini ya umri wa 18.

Mamlaka zinakanusha kuingilia mchakato wa kisiasa katika orodha ya wapiga kura,zikisisitiza kuwa zinaheshimu maamuzi ya mahakama huru.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us