Abel Kai: Kigugumizi si ulemavu kwangu
Abel Kai: Kigugumizi si ulemavu kwangu
Kinyume na dhana potofu za kawaida, kigugumizi hakihusiani na akili au woga. Mara nyingi huanza katika utoto na, kwa wengine, huendelea kuwa watu wazima.
11 Machi 2025

Mwendo wa madaha na madoidoi kwenye jukwaa la wanamitindo, ni kitu cha kawaida jioni nyingi kwa Abel Kai, mwanamitindo na modo wa kiume jijini Nairobi.

Kuonyesha mavazi ya kiume kutoka kwa wabunifu wanaoheshimika kote nchini katika maonyesho ya mitindo, vifaa vya kupambia na mikoba ya kiume.

Akiwa na urefu wa zaidi ya futi sita, matembezi yake ni ya haraka na ya kukokotwa na ya kuvutia sana. Lakini hali ni tofauti sana unapoketi naye kwa mazungumzo. Ana kigugumizi kizito sana.

‘’Nakumbuka wakati mmoja nikiwa shule ya Msingi niliombwa nisome sehemu ya kitabu kwa sauti darasani. Nilijitahidi kupata maneno,’’ anasema Abel. ‘’ Kigugumizi changu kilizidi kuwa mbaya, na nikaingiwa na mfadhaiko. Niligugumia sana hivi kwamba hatimaye nilitokwa na machozi,’’ anakumbuka.

Nlitaka kukubalika

Kigugumizi, ni ugonjwa wa usemi unaoathiri ufasaha, na kusababisha usumbufu katika mtiririko wa usemi.

Vikatizo hivi vinaweza kujitokeza kwa namna ya kujirudiarudia au kurefusha maneno, au vizuizi ambapo mtu anatatizika kutoa sauti au maneno fulani.

Lakini kwa Abel mtoto mdogo wakati huo akitafuta kufanana na wenzake, alihisi kama kisu kinachochoma na kusokota tumboni kila alipojaribu kuongea. Lakini anasema jambo baya zaidi kwake lilikuwa ni mtazamo wa rafiki yake waliposikia kigugumizi chake.

‘’Wakati wa mapumziko, wanafunzi wenzangu walijitenga nami, wakiamini kuwa kigugumizi changu kilikuwa cha kuambukiza. Nilitaka kujitetea, kueleza kwamba halikuwa jambo ambalo wangeweza "kupata," lakini kila jaribio la kuzungumza lilinifanya nipate kigugumizi zaidi,’’ Abel anaiambia TRT Afrika.

Sababu haijulikani

Ingawa sababu kamili bado haijaeleweka, kigugumizi kinaaminika kuwa kinatokana na mchanganyiko wa sababu za kijeni, neva na kimazingira.

Hali hii bado inawashangaza wataalam wa afya kwani bado hakuna dalili wazi ni nini kinachosababisha au jinsi ya kutibu, ingawa baadhi wameweza kudhibiti kupitia mazoezi ya usemi. Pia kuna matukio wakati kigugumizi kilipotea peke yake baada ya umri fulani.

Lakini Abel ambaye bado ana kigugumizi anasema kutojua hali hiyo ni sehemu ya tatizo katika jamii.

Anasema watu wanaona kigugumizi kwa juu juu tu lakini ni nadra sana kuelewa uzito wa kihisia unaoletwa nacho.

‘’Kugugumia ni kama jiwe la barafu—unaona sehemu ndogo tu juu ya uso, huku mapambano makubwa na magumu zaidi yakibaki yamefichwa chini. Zaidi ya ugumu wa usemi unaoonekana kuna ulimwengu wa kutojiamini, unyanyapaa, na hali ya kujiamini iliyovunjika,’’ anaongeza.

Kugugumia ni kama jiwe la barafu—unaona sehemu ndogo tu juu ya uso, huku mapambano makubwa na magumu zaidi yakibaki yamefichwa chini.

Abel Kai

Je, alipataje ujasiri wa kuingia katika maisha ya kutangazwa?

‘’Nilipokua, nilitambua kwamba kigugumizi si kitu ambacho ningeweza kufuta—ilikuwa ni sehemu yangu. Badala ya kuupinga, nilichagua kuukubali. Kukubalika huku hakukuwa rahisi, lakini kulinifunza ujasiri na kujitambua. Nilijifunza kuabiri hali tofauti za kijamii, nikijitayarisha kiakili kwa mazungumzo na kuandaa mikakati ya kukaa mtulivu,’’ Abel anaiambia TRT Afrika.

Hakuna uhusiano na akili

Zaidi ya kipengele cha kimwili, kigugumizi kinaweza kuathiri kujithamini na utangamano na jamii.

Wataalamu wanasema, kinyume na maoni potofu ya kawaida, kigugumizi hakihusiani na akili au woga.

‘’Hasira za kushindwa kutaja jina langu mwenyewe, fedheha ya kudhihakiwa shuleni, na woga wa mara kwa mara wa kuzungumza mbele ya watu umekuwa vita vyangu vya kimyakimya. Lakini sikuruhusu hilo linifafanulie maisha yangu. Nilifuzu kwa kiwango cha juu zaidi katika masomo yangu na kujisukuma kufanya kazi,’’ anajisifia kwa kujigamba.

Ingawa hakuna sababu mahususi inayojulikana inayosababisha kigugumizi, baadhi ya watu wamejulikana kuchochewa na tukio, sauti au ishara.

Nachagua kuelimishana

‘’Mojawapo ya changamoto kubwa ya kugugumia ni hali ya kihisia-moyo. Hasira na wasiwasi hufanya hali kuwa mbaya zaidi,’’ Abel anasema. ‘’Ninapokuwa na woga au kufadhaika, kigugumizi changu huongezeka, na kufanya mawasiliano kuwa magumu zaidi. Baada ya muda, nimejizoeza kuwa mtulivu, hata katika hali ngumu, kwa sababu itikio langu huathiri si mazungumzo tu bali pia jinsi watu wanavyoniona,’’ anaendelea kusema.

Watu wengi zaidi wanafahamu sasa kuhusu kugugumia kuliko tuseme miaka kumi au ishirini iliyopita. Lakini Abel anasema anaendelea kupigana kupitia harakati na uhamasishaji ili kupata uungwaji mkono zaidi.

‘’Licha ya maendeleo mengi, bado nakutana na unyanyapaa na kukosa subira kutoka kwa watu ambao wanashindwa kuelewa mapambano yangu. Kumekuwa na nyakati ambapo nilihisi kutoonekana, kunyamazishwa sio tu na hotuba yangu bali na hukumu ya wengine,’’ anasema.

‘‘Kwa hiyo, badala ya kuwa na hasira , nachagua kuelimisha.’’ anaambia TRT Afrika.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us