AFRIKA
2 dk kusoma
Idadi ya waliofariki kwenye mafuriko ya Afrika Kusini yafikia 67
Maafisa wa uokoaji wa Afrika Kusini wamepata miili zaidi, siku kadhaa baada ya mvua kubwa kunyesha katika mkoa wa Eastern Cape, na kufanya idadi ya waliofariki kufikia 67.
Idadi ya waliofariki kwenye mafuriko ya Afrika Kusini yafikia 67
Kumekuwa na baridi kali katika Mkoa wa Eastern Cape wa Afrika Kusini katika siku za hivi karibuni, / Picha: Reuters
12 Juni 2025

Maafisa wa uokoaji wa Afrika Kusini wamepata miili zaidi siku ya Alhamisi, siku kadhaa baada ya mvua kubwa kunyesha na upepo mkali katika mkoa wa Eastern Cape, huku idadi ya waliofariki ikifika 67.

Upepo mkali kipindi cha baridi kali uliathiri maeneo ya vijijini siku ya Jumatatu, kusababisha mito kupasua kingo zake na nyumba kuzama ndani ya maji, huku nyumba kadhaa ambazo hazijajengwa vizuri zikianguka.

Maeneo yaliyoathirika ni yaliyo karibu na mji wa Mthatha, karibu kilomita 800 kusini mwa Johannesburg, ambapo wakazi walirudi kwenye matope siku tatu baadaye kuokoa walichoweza katika nyumba zao zilizoharibika.

'Miili kadhaa imepatikana'

"Huku maji yakituwa, miili kadhaa inaendelea kupatikana," amesema Caroline Gallant, Meneja Shirika la Msalaba Mwekundu la Afrika Kusini eneo la Eastern Cape, ambalo limetuma msaada kwenye eneo lililokumbwa na majanga.

Nyumba zaidi 3,000 zimeathirika, ameliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa "ilikuwa janga baya zaidi kuwahi kutokea".

"Idadi ya waliofariki sasa imefika 67," Velenkosini Hlabisa, waziri wa vyama vya ushirika, utawala bora na masuala ya kijadi, aliwaambia waandishi wa habari.

Miili hiyo inajumuisha wanafunzi sita ambao walikuwa miongoni mwa 10 waliokuwa ndani ya gari la shule lililosombwa na mafuriko, alisema. Watoto wanne bado hawajapatikana, maafisa wanasema.

Watu wanahitaji msaada

"Idadi inatarajiwa kuongezeka zaidi," alisema Ali Sablay, msemaji wa wakfu wa Gift of the Givers, shirika la misaada ambalo limepeleka watu kusaidia katika eneo hilo.

"Katika kipindi cha saa 24 idadi ya watu wanaohitaji msaada imeongezeka kutoka 5,000 hadi 10,000," aliliambia shirika la habari la AFP.

Serikali imetoa wito kwa raia wa Afrika Kusini kuwa makini katika siku chache zijazo kutokana na kuwepo kwa "hali mbaya ya hewa" inatarajiwa kote nchini.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us